Siku ya Ijumaa, wakenya wameendesha kampeni maalamu ya upandaji miti nchini humo kuwakumbuka waathirika wa maafa ya mafuriko yaliyoua watu 230, na kuwaacha wengine 200,000, bila makazi.
Rais William Ruto aliweka malengo ya kupanda miti milioni 200 katika kuadhimisha siku hiyo na pia kuhuisha mkakati wa kutunza mazingira.
Watu mbalimbali, likiwemo baraza la mawaziri na watumishi wa umma waandamizi, waliongoza kampeni hiyo kwa kupanda miche ya miti katika maeneo yaliyoathiriwa na shughuli za binadamu.
Hata hivyo, hapakuwa na kiashiria chochote cha iwapo Rais alifikia lengo lake, hadi kufikia Ijumaa jioni.
Akiwa ameambatana na mkewe Rachel Ruto, Rais Ruto aliongoza kampeni hiyo ya kitaofa katika msitu wa Kiambicho ulioko katika kaunti ya Mùrang'a. Kulingana na Ruto, kampeni hiyo, itaendelea kwa miezi sita ijayo.
“Tunaishi kwenye uhalisia wa mabadiliko ya tabia nchi. Na ndio maana tumeacha leo, tumeamua kuacha shughuli zote kuja kupanda miti,” Ruto amesema.
“Ni lazima tutafute suluhisho la mabadiliko ya tabia nchi na suluhisho lenyewe ni upandaji wa miti.”
Kwa upande wake, Jeshi la Ulinzi la Kenya limesema kuwa maofisa wake wamepanda miche 10,000 katika kambi za mjini Nairobi.
Hapo awali, serikali ya Kenya imeendesha kampeni za upandaji miti ili kuhuisha misitu nchini humo. Hata hivyo, idadi ya miti iliyowahi kupandwa haijawahi kutolewa.
Siku ya Ijumaa, Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki alisema mabadiliko ya hali ya hewa yataainishwa kama moja ya vitisho vya usalama nchini Kenya, kama ilivyo kwa ugaidi.
"Tunachukulia mabadiliko ya hali ya anga na athari zake mbaya kama tishio la usalama wa taifa. Ni lazima turudishe mazingira yetu kwa kupanda miti ya kutosha kwa ajili ya uendelevu wa kiikolojia," alisema Kindiki wakati alipokuwa akiongoza kampeni ya upandaji miti katika kaunti ya Marsabit, kaskazini mwa Kenya.
"Ndani ya mwezi mmoja, nchi imepoteza watu 258 kutokana na mafuriko, karibu idadi ya watu waliouawa katika mashambulizi yote ya kigaidi yaliyotokea nchini," aliongeza.
Taasisi ya Kimarekani ya Masuala ya Afrika imempongeza Rais Ruto kwa kutangaza siku maalumu ya upandaji miti, kuwakumbuka waathirika wa mafuriko na pia kuahidi kutoa dola milioni moja kama msaada kwa waathirika wa janga hilo.
Hapo awali serikali ilitangaza mpango wa kuongeza ukubwa wa misitu hadi kufikia asilimia 30, ifikapo 2032, katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.