Kaulimbiu ya Siku ya Redio Duniani ya 2025 ni "Redio na Mabadiliko ya Tabianchi." /Picha: Reuters

Na Charles Mgbolu

Ishara ya taa nyekundu ya tuko hewani 'On Air' inawaka huku Micah Sunday, mtayarishaji wa Rhythm FM huko Lagos Nigeria, akiingia studio. Ana dakika 45 kabla ya taarifa ya kwanza ya habari siku hiyo kuanza hewani.

Ungefikiri kuwa amechanganyikiwa, lakini Micah hajachanganyikiwa. Ni siku nyingine tu yenye shughuli nyingi kwake ofisini.

Kama mojawapo ya vituo binafsi maarufu zaidi vya Nigeria, Rhythm FM inawakilisha uwepo wa redio katika nafasi ya akili ya msikilizaji huku kukiwa na kuenea kwa vyombo vya habari vya kidijitali.

Hakika, mawimbi ya redio yanaendelea kuvuma katika bara zima, yakichanganya muziki na burudani na simulizi muhimu - kutoka kwa mabadiliko ya hali ya hewa hadi uhusiano wa kijamii.

Tarehe 13 Februari, inayoadhimishwa duniani kote kama Siku ya Redio Duniani, ilikuwa na mada "Redio na Mabadiliko ya Tabianchi" ikisikika katika vituo kote barani Afrika na kwingineko.

Siku ya Redio Duniani ilianzishwa mwaka 2011. /Picha: Reuters

Matangazo ya habari ya Micah iliwatangaza wanaharakati wanaopigania hali ya hewa wakitumia redio kusambaza habari muhimu kuhusu hali ya hewa na kupigania uendelevu wa mazingira.

Kayode Bakerr, mkuu wa kikundi cha Redio katika Rhythm FM, anasema redio ina jukumu muhimu katika kutoa taarifa na kuelimisha wasikilizaji, hasa maeneo ya vijijini ambayo ni vigumu kuwafikia watu huko.

“Maeneo mengi ya vijijini bado yanategemea sana redio kwani kuna upenyezaji mdogo wa intaneti, na watu wengi hawana vifaa vya kisasa. Redio husaidia kuziba pengo muhimu la taarifa,” Bakerr anaiambia TRT Afrika.

Bado ni kifaa cha juu

Ili kuenzi ushawishi wa chombo hiki, UNESCO ilianzisha Siku ya Redio Duniani mwaka 2011.

Ili kuenzi ushawishi wa redio, UNESCO ilianzisha Siku ya Redio Duniani mwaka 2011.

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliidhinisha kama siku ya ukumbusho wa kimataifa mwaka uliofuata kwa taarifa ya kuisifu redio kama chombo chenye nguvu kinachostahili kusifiwa "kwa kusherehekea ubinadamu katika utofauti wake wote" na kutumika kama "jukwaa la mazungumzo ya kidemokrasia."

Katika mazingira ya vyombo vya habari vya Kiafrika, ufikiaji wa redio unaendelea kukua licha ya kuongezeka kwa umaarufu wa mitandao ya kijamii na akili mnemba.

Kulingana na utafiti uliochapishwa na Chuo Kikuu cha Oxford mnamo 2024, redio imekuwa maarufu karne moja baada ya kuonekana katika bara la Afrika hivi kwamba sasa ina "ushawishi mkubwa wa ulimwengu".

Afrobarometer, mtandao wa utafiti wa barani Afrika, unaripoti kuwa 68% ya Waafrika hupata habari zao kutoka kwa redio kila siku au kila wiki, wakati ni 53% tu wanapata habari zao kutoka kwa televisheni na 37% kutoka vyanzo vya mtandao.

Utafiti huo pia unaonesha kuwa umaarufu wa redio haukomei tu kwa nchi zilizo na viwango vya chini vya ufikiaji wa mtandao.

Kulingana na utafiti huo asilimia 80 ya Waafrika Kusini wanasikiliza redio angalau mara moja kwa wiki katika nchi ambayo vyombo vya habari vya kidijitali vina msingi mkubwa.

Kukomesha habari za uwongoKwa Moses Umanah, mkuu wa utayarishaji wa Televisheni ya Silverbird yenye makao yake mjini Lagos, vyombo vya habari vya jadi kama vile redio vinaweza kusaidia kupambana na taarifa potofu.

Kuna matumaini kwa redio na mustakabali wake kama chombo cha kusambaza habari. /Picha: Reuters

"Pamoja na taarifa potofu kuwa na uwezo wa kuenea kwa haraka katika mitandao ya kijamii, redio ni chombo chenye nguvu cha uthibitishaji kwa sababu taarifa hutolewa na mtu anayejulikana na wala si mtumiaji asiye na uso kwenye mtandao," Umanah anaiambia TRT Afrika.

Hata hivyo, wasimamizi wa vituo vya redio na watangazaji wanakiri kwamba chombo cha habari cha jadi kinakuwa hatarini kutokana na ujio wa mitandao ya kijamii yenye mamilioni ya watumiaji.

Utafiti pia unaonesha ushindani mkali kutoka kwa majukwaa ya kidijiti yanayoibuka kama vile podkasti, ambayo yamekuwa kwa kasi kubwa katika bara miaka ya hivi karibuni.

Kulingana na tovuti ya utafiti ya Statista, soko la podkasti barani Afrika linatarajiwa kufikia watumiaji milioni 35.7 ifikapo 2029. Kupenya kwa watumiaji katika soko hili kunatarajiwa kuwa 2.7% mnamo 2025.

Changamoto kubwa kwa redio ni kuvutia wasikilizaji wenye umri mdogo.

Micah Sunday anasema athari ya redio inaweza kupimwa kwa idadi ya umri wa wapiga simu ambao hushirikisha waandaji katika mazungumzo hewani. "Wapigaji simu ambao mara nyingi huchangia mazungumzo kwenye redio huwa ni watu walio na umri wa zaidi ya miaka 30. Inaonesha kuwa redio inahatarisha kupoteza mawasiliano na kizazi kipya ambacho kinapata maudhui kwenye majukwaa ya kidijitali ambayo kwa kawaida hayawezi kupata kwenye redio." Hata hivyo, kuna matumaini kwa redio na mustakabali wake kama chombo cha kusambaza habari.

"Redio inabaki katika nafasi ya kipekee ya kuleta jamii pamoja na kukuza mazungumzo chanya kwa mabadiliko. Kwa kusikiliza wasikilizaji wake na kuwapa wanachokipenda, huduma za redio hutoa maoni na sauti tofauti zinazohitajika kushughulikia changamoto ambazo sote tunakabiliana nazo," UN inasema.

TRT Afrika