Mwanablogu Pelumi Nub./Picha: Pelumi Nubi  

Akiwa anishi nchini Uingereza, mwanablogu huyo maarafu kutoka Nigeria anakabiliwa na tatizo la "ugumu wa kusoma" maarufu kama dyslexia, huku akiendelea kujizoelea umaarufu kupitia mitandao ya kijamii baada ya kuendesha gari mwenyewe kutoka Uingereza mpaka Nigeria.

Dyslexia ni tatizo ambapo muhusika anapata tatizo kwenye kuandika na kusoma na kutambua sauti za matamshi.

Pelumi Nubi, ambaye alitangaza safari yake kubwa ya barabarani mnamo Januari, alikaribishwa na maafisa wa Nigeria alipowasili kwenye mpaka wa Nigeria na Benin siku ya Jumapili baada ya safari ya siku 68.

Katika safari yake yote, aliandika changamoto zake nyingi kwenye mitandao ya kijamii.

Mashabiki wake waliokuwa wakimsubiria huku wakicheza na kupeperusha mabango, walikuwa wanamsubiria mwanamke huyo mwenye miaka 28, wakati akivuka mpaka wa Nigeria na Seme siku ya Jumapili.

Mamlaka za Nigeria zimemsifu Pelumi kwa ushujaa wake. Picha: Pelumi Nubi

Baadaye alipokelewa na maafisa wa Huduma ya Forodha ya Nigeria.

Safari yake ilitangazwa kupitia chaneli yake YouTube na kutangazwa na Gboyega Akosile, msemaji wa gavana wa Lagos.

Hata hivyo, ilibaki kidogo safari yake ihitimishwe vibaya baada ya gari alilokuwa akisafiria kupata ajali muda mfupi baada ya kuwasili Liberia.

Hofu kubwa iliwajaa mashabiki wake baada ya picha za gari hilo likiwa limeharibika vibaya kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.

Hata akiwa ndani ya gari la wagonjwa, Pelumi alipata wasaa wa kuwashirikisha mashabiki wake kilichomtokea na kuandika, "Niombeeni."

Aliendelea kupata matibabu hospitalini japo hakuwa tayari kuonesha picha za majeraha yake.

Alisafiri katika nchi 17. Kutoka Uingereza hadi Ufaransa, Uhispania, Morocco, na kupitia jangwa kubwa la Sahara.

Akiwa mwanamke anayeishi na ugonjwa wa dyslexia, Pelumu anasema nia yake haikuwa kuweka rekodi bali kuionesha dunia kuwa hakuna lisilowezekana.

Alindika kwenye ukurasa wake wa Instagram, ‘’Kama msafiri mwanamke mweusi pekee, nataka kuonesha kwamba matukio kama haya yanawezekana. Ni kuibua na kuweka wazi uzuri wa bara letu na kuwatia moyo baadhi yenu kufuatilia ndoto zenu pia.’

Pelumi aliweka wazi kuwa ilimchukua mwaka mmoja kupanga safari hiyo akiwa peke yake na alilala kwenye gari lake ili kupunguza gharama. Njia alizopitia:

‘’ Uingereza hadi Ufaransa, kisha Hispania, na kuelekea Morocco. Baada ya hapo, ni kupitia Jangwa la Sahara Magharibi, Mauritania, Senegal, Gambia, Guinea-Bissau, Guinea, Sierra Leone, Liberia, Mali, Burkina Faso, Côte d'Ivoire (Ivory Coast), Ghana, Togo, Benin, na hatimaye Nigeria, ikifika Lagos. Tutaona jinsi mambo yatakavyokuwa!’’ aliandika kwenye Instagram.

TRT Afrika