Na Mazhun Idris
Siku ya Jumamosi alasiri, Salmanu Sani Salihu mwenye umri wa miaka 14 ameketi akiwa amekunja miguu yake ndani ya kibanda kidogo - kituo chake cha kazi. Akiwa na uzi wa kahawia na sindano ndogo, anasuka kwa ustadi katika kitambaa cha rangi ya lilac.
Salmanu anaunganisha nyuzi nene za kudarizi juu ya mchoro wa penseli kwenye sehemu ya kanzu ya kiume iliyoshonwa nusu, na hivyo kutoa pambu zuri na mifumo ya nyuzi kupinda na kuremba.
Aliyeketi mukabala na yeye ni kaka yake mkubwa, mkufunzi wa kudarizi kwa mikono, Nuhu Sani Salihu. kijana huyo mwenye umri wa miaka 35 anamiliki duka la kudarizi ambalo liko katikati ya Soko maarufu la Zaria Kaskazini mwa jimbo la Kaduna, Nigeria. Wanatengeneza mavazi mbalimbali ya kitamaduni ya Kihausa.
"Kwa sababu hii ni wikendi, tunakuja kazini kabla ya saa sita mchana, na tutafunga saa kumi jioni," Salmanu, anaiambia TRT Afrika huku yeye na wafunzwa wengine wakizingatia kazi yao ya sindano na uzi.
Imejumuishwa katika mitaala ya shule
Salmanu alianza kujifunza urembeshaji wa mikono miaka minne iliyopita. Mchana wa leo, anafanya kazi na ndugu zake wengine wawili Abdulkadir na Jabir wote pamoja na vijana wengine wawili wanaojifunza kazi hii- Abdullahi na Abdulkarim.
Kupitia miaka ya kujifunza kudarizi kwa mikono, watoto hukua na kuwa wabunifu wa Utaalamu wa mitindo.
Kama watoto wengi Kaskazini mwa Nigeria, Salmanu anachanganya mafunzo ya ufundi stadi na kufuata elimu rasmi mazoezi ambayo hupunguza hatari ya kuwa bila kazi baada ya shule.
Anasoma shule ya Barewa, shule ya sekondari iliyoanzishwa mwaka 1921, ambayo ilitoa Waziri Mkuu wa kwanza wa nchi hiyo Abubakar Tafawa Balewa na wakuu wengine kadhaa wa nchi katika taifa hilo lenye watu wengi zaidi barani Afrika.
Salmanu tayari ameendelea katika mafunzo yake ya kudarizi - wakati mwingine anafanya kazi peke yake - ambayo inampa fursa ya kupata mapato. Hivi ndivyo ilivyo kwa wenzake pia.
"Ninafurahia kujifunza ufundi huu, na kwa pesa kidogo ninazopata mwisho wa kazi ya kila siku, nalipa sehemu ya gharama zangu za shule, na hata kusaidia familia yangu," Abdullahi Isyaku mwanafunzi mwingine anaiambia TRT Afrika.
"Nilinunua kitambaa cha nguo zangu na nikajipambia mwenyewe," Abdullahi anasema, akionyesha kitambaa alichovaa.
Katika siku za wiki, wakati shule inafungwa karibu saa saba mchana, watoto hurudi nyumbani kwa mapumziko mafupi ya chakula cha mchana na kisha kwenda kwenye duka la mafunzo ya kudarizi ambapo wanafanya kazi hadi saa kumi jioni wanapohudhuria madrassa ya jioni - shule ya Kiislamu.
"Baba yangu alinileta hapa kujifunza ufundi wa kudarizi, badala ya kucheza mitaani," Abdullahi anaelezea.
Watu wa Hausa wana tasnia ya ufumaji wa vitambaa ya milenia na ubunifu wa mitindo, inayodhihirika katika kaftan za kitamaduni na vazi linalotiririka liitwalo ‘babbar riga’, maarufu kote Afrika Magharibi na Kati.
Katika utamaduni wa Kihausa, mavazi haya ya kupambwa kwa mkono yanajulikana zaidi na wanaume, lakini kuna miundo fulani ya mavazi ya kawaida kwa wanawake pia. Kama mavazi, ufundi hupitishwa kutoka kizazi hadi kizazi.
Ingawa urembeshaji wa mashine, katika miaka ya hivi majuzi, umechukua sehemu ya soko kwani wabunifu wengine hutumia jiometri inayotengenezwa na kompyuta kubuni motifu tata, mavazi yaliyopambwa kwa mkono bado yanajulikana kwa kila kizazi na tabaka la jamii ikiwa ni pamoja na familia ya kifalme na wanasiasa.
Aina zote mbili , nguo zilizopambwa kwa mkono na zile za mashine zinauzwa nchini na pia kusafirishwa zaidi kwa diaspora za Kiafrika huko Ulaya na Asia.
Kama wengine katika tasnia ya mitindo, wapambaji wa kudarizi kwa mikono hupata ongezeko la ajabu la biashara wakati wa sherehe za msimu kama vile sherehe za Waislamu za Eid huku mahitaji ya mavazi mapya yakiongezeka.
Watoto kama Salmanu na Abdullahi wanaamini ufundi huo utawatayarisha vyema kwa siku zijazo pamoja na elimu rasmi na ya kidini wanayopata.