Maseneta wa Nigeria wametoa mishahara yao ya mwezi Disemba kwa waathiriwa wa shambulio la anga lililofanywa na jeshi la Nigeria.
Zaidi ya raia 80 waliuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa katika shambulio la ''ambalo halikutarajiwa'' dhidi ya mkusanyiko wa kidini katika kijiji cha Tudun Biri katika jimbo la Kaduna wiki iliyopita.
Kiasi kilichochangwa kilifikia N109 milioni ($137,945), kulingana na Naibu Rais wa Seneti, Barau Jibrin, ambaye alitoa tangazo hilo wakati wa ziara ya maseneta kwa gavana wa jimbo la Kaduna siku ya Jumapili.
Ismail Mudashir, msaidizi wa Seneta Jibrin, alisema pesa hizo zitatumwa kwa waathiriwa kupitia serikali ya jimbo.
Shambulio hilo limelaaniwa vikali, huku Rais wa Nigeria Bola Tinubu akikitaja tukio hilo kuwa la "kusumbua" .
Jeshi la Nigeria limeomba radhi kutokana na shambulizi hilo na uchunguzi umeamriwa na Rais Bola Tinubu.
Kumekuwa na matukio kadhaa sawia na hayo mashambulio ya kijeshi yanayowakumba raia nchini Nigeria huku wanajeshi wa nchi hiyo wakipambana na makundi ya wanamgambo na magenge ya utekaji nyara kaskazini mwa nchi hiyo.