Jeshi la Uganda linatafuta nyongeza ya zaidi ya dola milioni 103 (Sh381Bn) kama mtaji mpya wa kampuni ya kubeba mizigo ya Uganda Air Cargo.
Jeshi limeiambia Bunge kuwa fedha hizo zitaiwezesha kununua ndege mpya, ikidai kuwa injini ya ndege moja iliharibiwa na ndege, huku nyingine ikiwa imekwama eneo la vita nchini Sudan.
Shirika la Ndege la Uganda Air Cargo Corporation (UACC) lilianzishwa mwaka 1994, na ni mtoa huduma za usafirishaji wa mizigo kutoka mji wa Entebbe hadi maeneo ya Afrika Mashariki na Kati.
"Uganda Air Cargo ilikuwa na deni kubwa. Ndege mbili aina ya C130, moja kati ya hizo ilizuiliwa na haijawahi kufanyiwa kazi, ya pili ilikarabatiwa mwaka jana na baada ya kurudi, ndege aliingia kwenye injini kisha ikachukuliwa kwa ajili ya ukarabati ambao mpaka sasa haujakamilika," Donozio Kahonda mbunge wa Ruhinda Kusini aliliambia Bunge la nchi hiyo.
Kahonda alikuwa akiwasilisha taarifa ya Kamati ya Bunge ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Ulinzi mbele ya Kamati ya Bajeti ya Muongozo wa 2025/26 kwa Wizara ya Ulinzi.
"Na zile ndogo mbili, moja ilipata hitilafu huko Sudan na tumedai bima ili tupate nyingine lakini haijawezekana. Hata kuirejesha Uganda, kwa sababu iko katika eneo la vita, haijawezekana,” alibainisha Kahonda.
Kahonda alisema Baraza la Mawaziri lilipitisha agizo kwamba Uganda Air Cargo inapaswa kupewa Sh381Bn ili kupata ndege mpya kwa sababu nyingine ni kuukuu.
Aliongezea kuwa watengenezaji walishauri waangalie gharama za kuitengeneza dhidi ya gharama ya kupata mpya na pia waangalie uchakavu wa ndege, ambayo amesema inakadiriwa ilibaki na saa 40,000 kuisha.
Kahonda alisema kuwa watengenezaji walishauri kwa sababu ukarabati haukuwezekana, basi ingekuwa bora kupata mpya.
Hata hivyo, Dickson Kateshumbwa ambae ni Mbunge wa Manispaa ya Sheema alishangaa kwa nini walipakodi wa Uganda waendelee kufadhili Mashirika ya ndege ya Uganda Air Cargo na Uganda Airlines, badala ya mashirika hayo mawili kuunganishwa na kuokoa walipakodi gharama za kulipa leseni kwa ndege zisizofanya kazi.
"Jambo hili halifanyi kazi tunapendekeza tuiondoe. Vivyo hivyo kwa Polisi, ninaelewa kuwa Polisi wamepata ndege ambazo hazifanyi kazi na labda tunalipa leseni lakini hazifanyi kazi," Kateshumbwa alisema.
"Kuna hamu ya huduma hiyo lakini hakuna pesa. Tujikomboe kutoka kwa baadhi ya mambo ya hasara. Wizara aipe kampuni ya ndege ya taifa Uganda Airlines au iondoe na tusonge mbele. Kwa sababu unaposimamisha ndege unakuwa unalipa leseni,” alibainisha Kateshumbwa.