Idadi kubwa ya pomboo imepatikana imekufa kando ya fukwe moja nchini Somalia siku ya Ijumaa, tukio lililowaacha wakazi wa eneo hilo vinywa wazi.
Kulingana na wakazi wa eneo hilo, pomboo wapatao 100 walikuwa wamerundikana siku ya Alhamisi mchana, katika eneo la bandari ya Bossaso na fukwe ya Mareero kaskazini mwa jimbo la Puntland.
"Wizara ya mazingira na ile ya uvuvi zinaendelea kuchunguza tukio hili la kushangaza," ilisema serikali ya Puntland huku ikiahidi kutoa ripoti kamili kuhusiana na tukio hilo.
Ingawa idadi kamili ya pomboo waliokufa bado haijathibitishwa, wizara ya mazingira ya eneo inasema kuwa “wakazi wa eneo hilo wanakadiria kuwa huenda idadi ya pomboo hao ikafikia 100."
Hata hivyo, wizara hiyo ilipongeza hatua ya wakazi hao ambao walifanikiwa kuokoa pomboo 30 kwa kuwarudisha majini.