Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Kenya (DPP) ameitaka mahakama kuwezesha uchunguzi wa kiakili wa Sarah Wairimu Kamotho kabla ya kujibu shtaka la mauaji ya mume wake raia wa Uholanzi Tob Cohen.
Mahakama nchini Kenya imeamuru Sarah Wairimu azuiliwe katika gereza la Wanawake la Lang'ata hadi Januari 29 kuhusiana na mauaji hayo.
Taarifa za mauaji ya Cohen, raia wa Uholanzi zilisambaa nchini kote alipopatikana katika shimo la maji machafu nyumbani mwake Julai 2019. Wairimu alishtakiwa lakini kesi dhidi yake ikatupiliwa mbali baadaye 2022.
Wairimu alikamatwa tena siku ya Alhamisi baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka Renson Ingonga kusema sasa kuna ushahidi wa kutosha unaoonesha kuwa Wairimu alimuua Cohen usiku wa Julai 19 na 20, 2019, eneo la Lower Kabete, Kaunti ya Nairobi.
"Kufikishwa mahakamani kwa Wairimu kufuatia kukamatwa kwake Januari 23, ni baada ya kupokea taarifa mpya kuhusiana na kifo cha Cohen kutoka kwa Kurugenzi ya makosa ya jinai," alisema DPP katika taarifa iliyosambazwa kwenye mtandao wake wa X.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa pamoja na maelezo hayo mapya, DPP alitoa agizo la kusitishwa kwa uchunguzi wa jopo la mahakama kuhusu mauaji hayo ambalo lilikuwa limetolewa awali.
"Baada ya kufanya ukaguzi wa kina kuhusu taarifa mpya, Mkurugenzi wa Mashtaka amejiridhisha kwamba Wairimu alihusika katika kifo cha Tob Cohen," inaongeza taarifa yao.
Jaji Diana Kavedza aliagiza Wairimu apelekwe rumande katika gereza la wanawake la Lang' ata hadi tarehe 29 Januari 2025 atakapotoa uamuzi kuhusu suala hilo.
Mkurugenzi wa Mashtaka wakati wa mauaji, Noordin Haji mnamo 2022 alifuta shtaka la mauaji na kupendekeza kesi hiyo ifanyiwe uchunguzi na jopo la mahakama.
Alisema kuanzisha uchunguzi wa umma kutaruhusu watu kutoa taarifa zozote muhimu kuhusu mauaji ya Cohen kwa mamlaka, kama inavyotakiwa na sheria.
Lakini Mkurugenzi wa Mashtaka wa sasa Renson Ingonga ameagiza Sarah Cohen Wairimu afunguliwe tena mashtaka ya mauaji mahakamani.