Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameonya kwamba mzozo wa Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo unaosababishwa na mashambulizi ya waasi wa M23 unaelekea kuhatarisha vita vya kikanda.
UN imelaani kutekwa kwa mji mwingine wa kimkakati wa Sake, Mashariki mwa DRC.
Mapigano yamepamba moto zaidi katika eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo lenye utajiri mkubwa wa madini tangu mwanzoni mwa mwaka huu .
Kundi la M23 limedhibiti maeneo mengi zaidi katika eneo la Mashariki mwa DRC kuliko ilivyokuwa awali na kusababisha maelfu ya watu kuyakimbia makazi yao.
DRC na Umoja wa Mataifa wanaishutumu nchi jirani ya Rwanda kwa kuchochea uasi wa miaka mitatu wa M23 kwa kutumia wanajeshi wake na silaha. Rwanda inakanusha madai hayo.
"Mashambulizi haya yana madhara makubwa kwa raia na kuongeza hatari ya vita vya kikanda," msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric alisema Alhamisi.
Katibu Mkuu "anatoa wito kwa wahusika wote kuheshimu mamlaka na mipaka ya eneo la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kukomesha aina zote za uungaji mkono kwa vikundi vyenye silaha," Dujarric alisema.
Baada ya kuuteka mji wa Minova siku ya Jumanne, wapiganaji wa M23 wameendelea kusonga mbele, wakihamia mji wa Sake, karibu kilomita 20 kutoka mji wa Goma, mji mkubwa zaidi Mashariki mwa Congo.
Msemaji wa jeshi la taifa hajazungumzia kuhusu hali ya Sake siku ya Alhamisi, lakini taarifa ya Umoja wa Mataifa ililaani "kutekwa kwa hivi karibuni kwa Sake, hali ambayo inahatarisha zaidi mji wa Goma".
Kundi la M23 lilifanikiwa kudhibiti Goma kwa muda mfupi wakati wa uasi wa hapo awali mwaka 2012, na kusababisha wafadhili wa kimataifa kusitisha misaada kwa Rwanda. Hata wakati huo, waasi hawakushikilia msimamo wao kama walivyofanya sasa.