Tukio hilo limetokea huku waasi hao wakiendelea kusonga katika eneo lililokumbwa na machafuko./Picha: Reuters

Gavana wa kijeshi katika Jimbo la Kivu Kaskazini nchini DRC, amefariki dunia baada ya kupigwa risasi wakati wa shambulio lililofanywa na waasi wa M23.

Meja Jenerali Peter Cirimwami Nkuba, ambaye aliongoza jimbo hilo kuanzia mwaka 2023, aliuwawa siku ya Alhamisi, kulingana na vyombo vya habari vya AP na Reuters ambavyo viliinukuu ripoti ya Umoja wa Mataifa na maafisa wa serikali.

Tukio hilo limetokea huku waasi hao wakiendelea kusonga katika eneo lililokumbwa na machafuko.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, afisa huyo wa jeshi alijeruhiwa kwa risasi wakati akiongoza kikosi cha wanajeshi katika eneo lililo kilomita 20 kutoka mji wa Goma.

"Inaripotiwa kuwa alifariki asubuhi ya leo wakati akisafirishwa kutoka Goma kwa ajili ya matibabu zaidi," ilisema ripoti hiyo.

Mapigano yamezidi kuongezeka katika eneo lenye utajiri mwingi wa madini Mashariki mwa DRC toka kuanza kwa mwaka 2023, ambapo waasi wa M23 wamedhibiti eneo hilo.

Siku ya Ijumaa, kikundi cha Congo River Alliance (AFC), ambacho ni sehemu ya M23, kilisema kuwa kimepanga kutwaa eneo la Goma, lenye zaidi ya watu milioni 1.

DRC na Umoja wa Mataifa zimeituhumu nchi jirani ya Rwanda kwa kuchochea mapigano hayo, tuhuma zinazopingwa na Rwanda.

TRT Afrika