Na Emmanuel Onyango
Athari za tetemeko la ardhi lililotikisa jiji la Nairobi na mazingira yake zilisikika hata kwenye mitandao ya kijamii na kuzua mizaha ya kustaajabisha huku kukiwa na maandamano dhidi ya serikali nchini humo.
Eathquake Monitor ilitoa taarifa kupitia mtadao wa X, ilisema kitovu cha tetemeko hilo la ukubwa wa 4.7 kilikuwa kilomita 95 kusini magharibi mwa mji mkuu wa Kenya na "haikupaswa kusababisha uharibifu mkubwa".
Earthquake Monitor hutoa taarifa za wakati halisi kuhusu tetemeko la ardhi. liliongeza ya kuwa tetemeko hilo lilikuwa na kina kidogo sana cha kilomita 10 na lilisikika sana katika eneo hilo.
Lakini tetemeko hilo liliambatana na siku moja ya maandamano dhidi ya serikali nchini huku waandamanaji wakiendelea kumshinikiza Rais William Ruto ajiuzulu.
Takriban watu watatu waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika maandamano ya Jumanne, huku waandamanaji wakikabiliwa na vitoa machozi na risasi.
Waandamanaji wengi wanamlaumu Ruto kwa utovu wa uongozi, ufisadi na vifo vya makumi ya waandamanaji wakati wa maandamano ya awali dhidi ya serikali.
Sadfa ya tetemeko hilo na maandamano haikuwachwa nyuma kwenye mitandao ya kijamii.
Wakenya kwenye mitandao ya TikTok na X wamependekeza kwamba tetemeko hilo lilikuwa ''ujumbe kutoka juu'' kwa serikali, huku wengine wakitoa maoni juu ya sababu zingine "halisi" za tetemeko hilo.
Wengine kwa dhihaka walidai tetemeko hilo lilikuwa sauti ya Zakayo - neno la Kiswahili kwa mtu wa Biblia Zakayo - akishuka chini ya mti baada ya kukutana na Yesu.
Kuondoa shaka
Zakayo ni jina la utani la Rais William Ruto ambaye amefananishwa na mtoza ushuru wa kibiblia kutokana na pendekezo lake ambalo limesitishwa la kuongeza ushuru.
Hapo awali, rais wa Kenya alisema alikuwa hana shida kupachikwa jina la utani la Zakayo.
Hata hivyo, wataalam wanasema tetemeko hilo lilikuwa tukio la asili la kijiolojia ambalo halina uhusiano wowote na mvutano uliopo kati ya mamlaka na waandamanaji.
''Hii ilikuwa mojawapo ya zile zinazotarajiwa kutokea katika eneo la Bonde la Ufa nchini Kenya, lakini hii ilikuwa juu kidogo kwa ukubwa kuliko inavyotokea kawaida.
Haikuwa jambo la kawaida lakini si haba,'' Gladys Kianji, mtaalamu mkuu wa seismologist katika Chuo Kikuu cha Nairobi aliiambia TRT Afrika.
Mtaalamu huyo wa matetemeko aliondoa shaka kuhusu utani wa kustaajabisha ambao baadhi ya Wakenya walifanya kuhusu tetemeko hilo wakihusisha na maandamano.
'Tuwe makini'
''Ni sadfa tu kwamba ilitokea wakati wa maandamano yanayoendelea. Kisayansi hakuna uhusiano, hili lilikuwa ni jambo la asili na hakuna mwenye mamlaka juu yake na linaweza kutokea wakati wowote,'' alisema.
Kenya iko kwenye Bonde Kuu la Ufa la Afrika Mashariki, lakini haijawahi kushuhudia matetemeko makubwa ya ardhi.
''Matetemeko ya ardhi hayatabiriki lakini tunajua kutokana na rekodi kwamba matetemeko makubwa hutokea. Kenya imewahi kupata ukubwa wa 6.9 mwaka wa 1928 huko Subukia. Tunahitaji tu kujua tunaishi katika eneo hai na tunatakiwa kuwa makini,'' Kianji aliongeza.