Kiongozi wa upinzani Kenya Raila Odinga asema kutakuwa na maandamano kwa siku tatu / Photo: Reuters

Ujumbe kutoka kwa kiongozi wa muungano wa upinzani , Azimio Raila Odinga ni kwamba,

"Kuanzia Jumatano, uwe tayari kwa maandamano ya kuleta mabadiliko"

Kauli hii imezua hisia tofauti nchini Kenya.

"Mimi ni mzazi wa watoto wawili, nimeamua sitawapeleka watoto shuleni kwa hizo siku tatu kwasababu nahofia usalama wao," asema Mary Nafula , mkazi wa jiji la Nairobi.

"Mimi niko na biashara hapo mjini ya kuuza nguo , itanilazimu kufunga kibanda changu kwa siku tatu ,kwa sababu wiki iliyopita wakati wa maandamano hakukuwa na biashara yoyote," Edgar Wesonga mfanyabiashara jijini Nairobi amesema.

Wananchi wanaounga mkono wito wa maandamano wa kiongozi wa upinzani wanasema wako tayari Jumatano kuonyesha serikali ya rais William Ruto kuwa hawajaridhishwa na sera zake.

Katika mitandao ya kijamii kuna majadiliano moto huku watu wakipanga vile watajitosa mijini kwa ajili ya maandamano.

Maandamano yanayoongozwa na upinzani yamekuwa yakipinga ongezeko ya gharama ya maisha.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kutetea Haki za Binadamu imeonya maafisa wa serikali dhidi ya kutumia nguvu na risasi kwa waandamanaji.

"Ripoti zinasema kuwa hadi watu 23 wameuawa na dazeni kadhaa kuumizwa katika maandamano katika ya wiki iliyopita," ofisi hiyo ya Umoja wa Mataifa umesema.

Serikali inasema lazima sheria ifuatwe katika maandamano kuhakikisha hakuna vifo au uharibifu wa mali / Picha: Reuters 

Tamko kutoka kwa Polisi

Inspekta Jenerali, Japhet Koome amefahamisha umma kupitia taarifa kwamba maandamano yoyote ambayo yatafanyika sehemu yoyote ya Kenya kuanzia Jumatano tarehe 19 yatashughulikiwa kwa haraka.

Taarifa hiyo ilisema ingawa polisi wanatambua haki ya kikatiba ya maandamano hayo, matokeo ya hivi karibuni ni ishara tosha ya kwamba ni tishio kwa usalama wa taifa.

Waziri wa Usalama na Mambo ya Ndani Kithure Kindiki alisema serikali haijapiga marufuku mikutano ya hadhara na mikusanyiko, lakini sheria lazima ifuatwe,

"Sheria ya utaratibu wa umma inaruhusu wazi mikutano hiyo kufanyika kati ya saa kumi na mbili asubuhi na saa kumi na mbili jioni. Hata hivyo, yeyote anayepanga kusababisha machafuko, kuhujumu uchumi, na kujihusisha na ukiukaji wa sheria atashughulikiwa kwa uthabiti na madhubuti, kwa mujibu wa sheria," Kindiki alisema.

Baada ya maandamano Jumatano iliyopita, polisi walisema maafisa waliripoti uchovu na kuwa na changamoto ya kutokuwa na vifaa vya kutosha vya kuzuia ghasia.

Mabalozi wa nchi 13 wametoa taarifa ya pamoja wakiomba amani nchini Kenya. Nchi zilizochangia ni pamoja na Australia, Marekani , Uingereza, Denmark , Sweden na Uholanzi.

"Tunatambua matatizo yanayowakabili wakenya wengi na tunazitaka pande zote kuwasilisha na kusuluhisha matakwa yao kwa amani ili kujenga taifa kwa pamoja na kuhakikisha hakuna vifo zaidi," imesema taarifa yao.

Mmoja wa viongozi wa muungano wa Azimio Kalonzo Musyoka amedai " kuna kikosi ambacho kimepanga kuwauwa watu kesho katika maandamano na katika maandamano mengine yajayo."

Katika taarifa kwa vyombo vya habari viongozi hao wameambia serikali ya Rais Ruto kwamba.

"Usituulize suluhu, fungua njia kwa utawala ambao una masuluhisho."

Sheria ya fedha 2023

Maofisa wa usalama wamelaumiwa kwa kutumia nguvu dhidi ya waandamanaji / Picha: Reuters 

Kati ya maswala ambayo waandamanaji wanapinga ni kutekelezwa kwa sheria ya fedha 2023 ambayo imependekeza ongezeko la ushuru.

Serikali inasema ni lazima kuongeza mapato ya ndani ya nchi lakini wanaopinga wanasema hii itaongeza gharama ya maisha.

Sheria hii ilifaa kuanza kutimizwa tarehe mosi Julai lakini haikuwezekana kwa sababu wafungua mashtaka wawili walienda mahakamani.

Seneta wa Busia, Okiya Omtatah, na muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya wamedai hakukuwa na ushiriki wa wananchi, na kwamba sheria hiyo haifai kuruhusiwa kwani ingeathiri wakenya wengi wanaoteseka.

Sasa Jaji Mkuu Martha Koome ameteua majaji watatu kusikiliza na kuamua kesi hii inayopinga Sheria ya Fedha ya 2023.

TRT Afrika