Leo, Jumatano, ni siku ya kwanza ya maandamano ya siku tatu ambayo yalipangwa na upande wa Upinzani.
Kinara wa Upinzani wa muungano wa AZIMIO, Raila Odinga alisema kuwa yatakuwa "maandamano ya kuleta mabadliko."
Serikali imesema maandamano hayo si halali na imeonya kuwa watakaoleta vurugu wataadhibiwa kisheria.
Kamati ya maaskofu wa Katoliki nchini Kenya imeomba utulivu nchini , huku maandamano ya siku tatu yakianza katika sehemu tofauti ya nchi .
"Tumejitahidi kuwaomba viongozi - rais na kiongozi wa upinzani kufanya amani na kukomesha mzozo huu," Askofu mkuu Martin Kivuva amesema katika taarifa yake kwa waandishi wa habari.
Maaskofu pia wanamataka rais William Ruto kubatilisha sheria ya fedha 2023, ambayo bunge ilipitisha Juni.
Sheria hii imefanya mabadiliko ambayo yataongeza ushuru katika sekta tofauti huku serikali ikitazamia kuongeza mapato ya ndani .
"Sheria ya fedha iliyotungwa hivi majuzi inawatwika mzigo mkubwa wananchi walio katika majonzi hasa wale wa kipato cha chini," ameongezea askofu mkuu Antony Muheria," kwa hiyo tunaomba rais abatilishe sheria ya fedha na kuanzisha mchakato utakaolenga kufikia malengo sawa ndani ya muktadha wa uchumi wa sasa."
Maandamano yaanza licha ya onyo
Maafisa wa usalama waliimarisha doria katika miji tofauti nchini mapema asubuhi kuhakikisha kuwa maandamano hayafanyiki.
Wizara ya elimu ikatangaza kuwa shule zitafungwa katika miji mitatu , Nairobi, Kisumu na Mombasa.
"Wizara ya elimu itatangaza kuanza tena kwa masomo katika shule zilizotajwa baada ya kutathmini hali ya usalama siku ya ya Jumatano," wizara imesema katika taarifa.
Shirika la reli la Kenya limetangaza kusitisha huduma za treni jijini Nairobi siku ya Jumatano kutokana na maandamano hayo.
Katika maandamano ya awali takriban watu 13 waliripotiwa kuuawa kulingana na wanaharakati wa kutetea haki, na watoto wa shule 53 walikimbizwa hospitalini baada ya kudaiwa kurushiwa mabomu ya kutoa machozi darasani mwao na polisi.