Rais wa Kenya William Ruto yuko nchini Ghana kwa ziara rasmi ambapo anafanya mazungumzo na rais mwenzake wa Ghana Akufo-Addo / Picha kutoka Ikulu Kenya

Serikali ya Ghana itaiunga mkono Kenya katika juhudi zake za kutaka uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika.

"Kaka yangu Rais Akufo-Addo nakushukuru sana kwa kukubali kuiunga mkono Kenya katika nafasi ya Uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika 2025-2028," Rais wa Kenya William Ruto alisema katika mkutano na waandishi wa habari mjini Accra, akiwa na rais wa Ghana.

Rais wa Kenya William Ruto kwa sasa yuko Accra kwa ziara rasmi ambapo anafanya mazungumzo na rais mwenzake wa Ghana ili kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, kibiashara na kihistoria.

Kenya inagombea uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika kupitia kiongozi wa upinzani nchini humo, Raila Odinga.

Umoja wa Afrika tayari umesema kuwa muhula huu uenyekiti utachukuliwa na kanda ya Afrika Mashariki. Hata hivyo Kenya ni lazima ijitahidi kupata angalau theluthi mbili ya kura za viongozi wa nchi 55 za Afrika, ili kuchukua nafasi hiyo.

Hadi sasa hakuna nchi nyengine Afrika Mashariki ambayo tena imewasilisha mgombea.

Wakati huo huo, Rais Ruto aliihakikishia Ghana kuwa Kenya itaiunga mkono kuwania kwa Bi Shirley Botchwey, Waziri wa Kigeni na Ushirikiano wa Kikanda, kwa nafasi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola kwa kipindi cha 2024-2029.

Kenya na Ghana zimetia saini mikataba saba inayolenga kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili.

Rais William Ruto alisema makubaliano hayo, yakiwemo baadhi yaliyotiwa saini na vyama vya wafanyabiashara kutoka Kenya na Ghana, yanalenga kuwezesha biashara na uwekezaji kati ya mataifa hayo mawili.

Lengo, alisema, ni kupanua fursa za kibiashara katika sekta binafsi kati ya watu wa mataifa hayo mawili.

TRT Afrika