Na Edward Qorro
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inaongoza kwa kupokea misaada mikubwa ya kifedha kutoka nchi zilizoendelea, ripoti ya taasisi ya Mo Ibrahim imesema.
Ripoti hiyo, iitwayo Financing Africa: Where is the Money?, inaonesha kuwa nchi hiyo kubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki ilipokea dola bilioni 3.4 kati ya mwaka 2013 hadi 2022.
Utafiti huo pia unatoa uchanganuzi wa kina wa mahitaji yote ya kifedha yanayoonekana kuwa muhimu kwa Afrika kukidhi mahitaji yake malengo ya maendeleo na hali halisi ya rasilimali zilizopo.
Pia inaonesha namna bara la Afrika linavyoendelea kutemegea misaada ya kifedha kutoka nchi kubwa duniani.
Kulingana na ripoti hiyo, Afrika ina rasilimali nyingi na za kutosha, lakini inakosa utaratibu ufaao wa namna ya kuzigawa na mara nyingine zinatumika vibaya.
"Fedha nyingi zinazotoka mataifa ya magharibi zinaelekezwa kwenye sekta za afya na elimu japo huja na masharti kadhaa," imesomeka sehemu ya tafiti hiyo.
Wakati DRC inashika nafasi ya kwanza kwa utegemezi wa fedha za misaada kutoka nchi za magharibi, Kenya iko katika nafasi ya pili, ikiwa imepokea dola bilioni 3.3.
“Tunahitaji mabadiliko ya kimtazamo. Hili halihusu Afrika kutembeza bakuli kwa nchi zilizoendelea. Kama ripoti inavyoonesha, pesa zipo lakini changamoto ni namna gani pesa hizi zinatumika kutatua matatizo yetu. Ni vyema kuchukua hatua na kufanya mageuzi kwa maslahi ya watu wetu,” amesema mwenyekiti wa taasisi ya Mo Ibrahim, Mohammed Fathi Ahmed Ibrahim katika ripoti hiyo ya hivi karibuni.
Kwa upande wake, Tanzania ilipokea dola bilioni 3 wakati Uganda ilipewa dola bilioni 2.4.