Djibouti imemteua Waziri wake ya Mambo ya Nje Mahamoud Ali Youssouf kuwania uenyekiti wa Tume ya AU / Picha: AFP

Mwezi Aprili 2024 Djibouti iliingia katika kinyanganyiro cha kuwania nafasi ya uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika.

Nchi hiyo imemteua Waziri wake ya Mambo ya Nje Mahamoud Ali Youssouf, aliyezaliwa Septemba 1965.

Iwapo Djibouti itashinda nafasi ya uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika ambayo ni ya uongozi wa sekretarieti ya AU, basi itahudumu kati ya 2025 hadi 2028.

Serikali ya Djibouti imemsifu Youssouf kuwa ni mtu wa tajriba ya zaidi ya miongo miwili kama Waziri wa Mashauri ya Kigeni inayomfanya mgombea bora zaidi katika nafasi hiyo.

Pia imemtaja kama mwanadiplomasia mzoefu, anayejua masuala za umoja wa Bara na uwezo wa kutumikia na kutoa sura mpya katika Shirika la kiafrika.

Youssouf ambaye anazungumza Kifaransa, Kiingereza na Kiarabu kwa ufasaha, amehudumu katika serikali ya Djibouti kama Waziri wa Mambo ya Nje tangu 2005.

Alifanya kazi katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Djibouti akiongoza idara ya masuala ya Kiarabu katika miaka ya 1990. Vile vile amewahi kuhudumu kama balozi wa Djibouti nchini Misri kuanzia 1997 hadi 2001.

Mwezi Julai 2001, Youssouf aliteuliwa kama Waziri-Mjumbe wa Ushirikiano wa Kimataifa na Mei 2005, aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Kulingana na sheria za Umoja wa Afrika ni fursa ya eneo la Afrika Mashariki kutoa mwenyekiti wa Tume ya AU. Djibouti sasa ni nchi ya tatu kuonyesha nia ya nafasi hii baada ya Kenya na Somalia.

Kenya imemteuwa waziri wake mkuu wa zamani Raila Odinga huku Somalia imemteua Fawzia Yusuf Haji Adam, waziri wake wa zamani wa mambo ya nje. Marais wa nchi za Afrika watakutana kufanya uchaguzi Februari 2025.

Kampeni bado zinaendelea. Pengine ni suala la kusubiri na kuona iwapo kuna nchi nyengine kutoka Afrika Mashariki ambazo zitaingia katika kinyang'anyiro hicho cha uenyekiti wa Tume ya AU.

TRT Afrika