Raila Odinga ni mmoja wa viongozi wenye ushawishi mkubwa Afrika kutetea haki za Wapalestina/ Picha Reuters. 

Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya na kinara wa muungano wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga, ameishtumu Israel kwa uvamizi dhidi ya raia wasiokuwa na hatia wa Palestina huku akitoa wito wa kusitishwa kwa mauaji yanayoendelea Gaza.

"Nikiwa hapa Mombasa, nataka kutoa ushauri kwa bwana Netanyahu, Netanyahu, Netanyahu, wacha kuua watoto wakiarabu wa Palestine," Raila amesema.

"Lazima tulaani kwa maneno makali iwezekanavyo, ukatili uliokosa ubinadamu ambao watoto na wanawake wasio na hatia, wananyanyaswa na utawala wa Netanyahu. Ni unyama," Raila Odinga ameongeza.

Aidha, Odinga ametoa wito kwa rais William Ruto kutosalia kimya dhidi ya Wapalestina.

Rais William Ruto alikuwa mmoja wa viongozi wa ulimwengu kusimama na Israel kufuatia uvamizi wa Oktoba 7.

"Bwana Ruto, usipotoshwe kulaani ndugu na dada zako mwenyewe, usinyamaze mbele ya unyama unaofanywa dhidi ya watu wa Palestina. Serikali ya Kenya lazima isimame na wanaoonewa. Lazima isimame na watu ambao wanafanyiwa ukatili, la sivyo, historia itakuhukumu, " Raila alisisitiza.

"Kenya inajiunga na ulimwengu wote kwa mshikamano na Serikali ya Israeli na inalaani bila shaka ugaidi na mashambulio dhidi ya raia wasio na hatia," Rais Ruto aliandika kwenye ukurasa wake wa X.

Kufikia siku ya jumapili, idadi ya vifo kutokana na uvamizi wa Israel katika ukanda wa Gaza tangu Oktoba 7 imefika watu 9,500, wakiwemo watoto 3,900 na wanawake 2,509," Salama Marouf, mkuu wa ofisi ya vyombo vya habari ya Gaza, alisema katika mkutano na waandishi wa habari. Wakati huo huo, Waisraeli 1,540 wameuawa.

TRT Afrika