Viongozi wa nchi za Mamlaka ya Kiserikali juu ya Maendeleo, IGAD wamekutana Djibouti kwa mkutano wao wa 41 wa kawaida.
Wanachama wa IGAD ni Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Somalia ,Sudan Kusini, Sudan Kenya na Uganda.
Mkutano huo umehudhuriwa na marais wa Djibouti Ismaïl Omar Guelleh, Somalia Hassan Sheikh Mohamud, Kenya William Ruto na waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed. Marais wa nchi zingine walituma wawakilishi,
Ajenda yao kuu ni mzozo unaoendelea nchini Sudan tangu 15 Aprili mwaka huu. Jeshi la Sudan na kikundi cha Rapid Support Forces zimekuwa zikipigana.
" Mkutano ni kuhusu hali ya dharura nchini Sudan kama sehemu ya juhudi za pamoja za AU/IGAD kushawishi pande husika kusitisha vita na kuruhusu mchakato wa kisiasa wa kuijenga upya nchi hiyo," mwenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat alisema katika akaunti yake ya X, alipowasili Djibouti.
Tangu mapigano kati ya Jeshi la Sudan (SAF) na Kikosi cha Rapid support Forces yazuke, katikati ya Aprili, Umoja wa mataifa, unasema takriban watu milioni 6.6 wamekimbia makazi yao na kukimbilia ndani na nje ya nchi, huku watoto wakiwakilisha karibu nusu ya idadi hii.
" Mzozo wa Sudan ndio mzozo mkubwa zaidi wa watu kuhama makazi. Huku watu wengi wakikimbia kuvuka mipaka, jumuiya zinazowakaribisha katika nchi jirani zinatatizika," anasema Clementine Nkweta-Salami, Mratibu wa UN wa Misaada ya Kibinadamu,
"Kuendelea kwa vita nchini Sudan kunaweza kuingiza eneo lote katika janga la kibinadamu. Hatuwezi kuruhusu hilo kutokea," anaongezea.
Shirika la data ya maeneo ya mizozo linalojulikana kama Armed Conflict Location & Event Data Project (ACLED) inasema kuwa inakadiria kuwa zaidi ya watu 12,190 wameuawa tangu mapigano yalipozuka mwezi Aprili, ikiwa ni pamoja na watu 1,300 waliouawa kati ya 28 Oktoba na 24 Novemba.
" Raia wenzetu katika Jamhuri ya Sudan wanaendelea kubeba mzigo wa mzozo huu wa muda mrefu, na ni wajibu wetu wa kimaadili kuharakisha utekelezaji wa maazimio ya sehemu ya makubaliano ya Jeddah, ambayo yameratibiwa na IGAD chini ya uongozi wake Ufalme wa Saudi Arabia na Marekani," Workneh Gebeyehu, katibu mkuu wa IGAD aliambia mkutano huo.
Mazungumzo ya amani katika ya jeshi la Sudan na kikundi cha Rapid Support Forces yamegonga mwamba.
"Mazungumzo ya amani na heshima yanasalia kuwa msingi wa mtazamo wetu, na ni kupitia juhudi endelevu katika mwelekeo huu ndipo tunaweza kuandaa njia ya amani ya kudumu," Gebeyehu ameongezea.
Rais wa Djibouti Ismail Omar Guelleh ameambia viongozi wenzake kuwa kunyamazisha binduki nchini Sudan si chaguo, ni lazima.
" Lazima tusisitize kuanzishwa mara moja kwa makubaliano ya kusitisha mapigano, kunyamazisha bunduki ambazo zimeharibu maisha ya raia wasio na hatia, kaka na dada zetu katika Jamhuri ya Sudan," Rais Guelleh amesema.
" Ni jukumu letu kuweka juhudi ya kufikia makubaliano mwafaka ambaye itahakikisha vita vinakwisha, uwezekano wa misaada ya kibinadamu kufikia watu na mafumo wa majadiliano kuweka musitishaji wa vita ni muhimu sana,"