Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limesitisha kwa muda wa miezi mitatu zoezi la kuondoka kwa wanajeshi wa Umoja wa Afrika kutoka Somalia.
Uamuzi huo unafuatia ombi la Somalia kutaka vikosi hivyo kusalia nchini humo kusaidia katika mapambano dhidi ya kundi la al-Shabab.
Ombi la Somalia liliungwa mkono na Umoja wa Afrika, nchi zote zinazochangia wanajeshi katika kikosi hicho na baraza lililokubali kuchelewesha kuondoka kwa wanajeshi 19,000 wa AU kwa siku 90.
Mwaka jana mwezi wa Aprili, Baraza hilo kwa kauli moja liliidhinisha kikosi kipya cha mpito kinachojulikana kama ATMIS, kusaidia Wasomali hadi pale vikosi vyao vitakapowajibika kikamilifu kwa usalama wa nchi hiyo mwishoni mwa 2024.
Vita vyaongezeka
ATMIS ilichukua nafasi ya Ujumbe wa Umoja wa Afrika nchini Somalia, inayojulikana kama AMISOM, ambayo imekuwa katika taifa hilo kwa miaka 15 kusaidia ujenzi wa amani nchini Somalia.
Hata hivyo, kikosi kipya kilipaswa kuondolewa kwa awamu, kuanzia Juni mwaka jana, wakati wanajeshi 2,000 walipoondoka Somalia na kukabidhi kambi sita za operesheni kwa vikosi vya usalama vya Somalia.
Awamu ya pili ya uondoaji huo ilianza mnamo Septemba kulingana na U.N. azimio ambalo linatarajia uondoaji kukamilika ifikapo Desemba 2024.
Serikali ya Somalia mwaka jana ilianzisha "vita kamili" dhidi ya al-Shabab ambayo inadhibiti sehemu za vijijini katikati na kusini mwa Somalia.