Umoja wa Mataifa waondoa vikwazo vya silaha vilivyodumu kwa miongo kadhaa kwa Somalia

Umoja wa Mataifa waondoa vikwazo vya silaha vilivyodumu kwa miongo kadhaa kwa Somalia

Vikwazo vya silaha viliwekwa mwaka 1992 kufuatia vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Somalia.
Umoja wa Mataifa uliondoa vikwazo vilivyowekwa kwa Somalia zaidi ya miaka 30 iliyopita. Picha: AA

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipiga kura kwa kauli moja siku ya Ijumaa kuondoa vikwazo vya mwisho vya kuuza silaha kwa serikali ya Somalia na vikosi vyake vya usalama, zaidi ya miaka 30 tangu kuwekewa vikwazo vya silaha kwa mara ya kwanza nchini humo.

Baraza hilo liliiwekea vikwazo Somalia mwaka 1992 kupunguza mtiririko wa silaha kwa wababe wa kivita waliokuwa wakihasimiana, ambao walikuwa wamemuondoa dikteta Mohamed Siad Barre na kuitumbukiza nchi hiyo ya Pembe ya Afrika katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Chombo hicho chenye wanachama 15 kilipitisha maazimio mawili yaliyoandaliwa na Uingereza: moja la kuondoa vikwazo kamili vya silaha kwa Somalia na lingine kuweka tena vikwazo vya silaha kwa wanamgambo wa al Shabaab wenye mafungamano na al Qaeda.

Silaha hatari

Azimio la kuondoa vikwazo vya silaha linaeleza "kwa ajili ya kuepuka shaka, kwamba hakuna vikwazo vya silaha kwa Serikali ya Shirikisho la Jamhuri ya Somalia."

Pia inaelezea wasiwasi wake kuhusu idadi ya vituo salama vya kuhifadhia risasi nchini Somalia, na inahimiza ujenzi, ukarabati na matumizi ya maghala salama ya risasi kote nchini Somalia. Inahimiza nchi zingine kusaidia.

"Kuondolewa kwa vikwazo vya silaha kunatuwezesha kukabiliana na vitisho vya usalama," alisema Balozi wa Somalia wa Umoja wa Mataifa Abukar Dahir Osman.

"Pia inaturuhusu kuimarisha uwezo wa vikosi vya usalama vya Somalia kwa kupata silaha na vifaa hatari ili kulinda ipasavyo raia wetu na taifa letu."

Kuimarisha usalama

Al Shabaab imekuwa ikiendesha uasi wa kikatili dhidi ya serikali ya Somalia tangu mwaka wa 2006 ili kujaribu kuanzisha utawala wake wenyewe kwa kuzingatia tafsiri kali ya sheria ya Kiislamu.

Serikali ya Somalia ilikuwa imeomba kwa muda mrefu vikwazo vya silaha viondolewe ili iweze kuimarisha vikosi vyake kukabiliana na wanamgambo hao. Baraza la Usalama lilianza kwa kiasi fulani kuondoa hatua za vikosi vya usalama vya Somalia mnamo 2013.

Rais Hassan Sheikh Mohamud alisema wiki iliyopita kwamba Somalia ina mwaka mmoja wa kuwatimua al Shabaab, huku muda wa mwisho wa wanajeshi waliosalia wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika kuondoka ukikaribia Desemba 2024.

TRT World