Somalia imeanzisha utoaji wa vitambulisho vya kwanza vya kitaifa tangi taifa hilo kuporomoka miongo mitatu iliyopita baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha kuanguka kwa serikali mnamo 1991.
Mamlaka ya Vitambulisho vya Kitaifa na Usajili (NIRA) imesema inalenga kusajili angalau Wasomali milioni 15 ifikapo 2026.
Rais Hassan Sheikh Mohamud na Waziri Mkuu Hamza Abdi Bare walikuwa wa kwanza kukabidhiwa vitambulisho siku ya Jumamosi.
"Hii ni siku ya kihistoria kwa taifa letu... nambari hii ya kitambulisho itatumika kama hati ya kitambulisho kwa kila mtu hadi kifo, " Rais Hassan Sheikh Mohamud alisema baada ya kupokea kitambulisho chake.
Mchakato wa kujenga upya
Uzinduzi wa vitambulisho ni katika Mchakato wa Ujenzi wa nchi ya Somalia na hatua muhimu kuelekea uchaguzi uliopangwa kufanyika 2026. Nchi hiyo kwa sasa inatumia mfumo wa kisiasa usio wa kura ya kuhesabu kura ya raia mmoja mmoja.
Bila vitambulisho vya taifa, Wasomali wamekuwa wakifanya shughuli za kibiashara ikiwa ni pamoja na huduma za benki na uhamisho wa pesa kupitia uaminifu na wakati mwingine kutumia pasipoti au hati ya kusafiria.
Upatikanaji wa huduma za serikali kama elimu na huduma za matibabu imekuwa pia ni kupitia mahusiano ya kijamii.
Hali hiyo imekuwa changamoto kwa usalama kwani kuwatambua waathiriwa na wahalifu wa vitendo vya kigaidi imekuwa ngumu mno.
Rais alitaja vitambulisho vya taifa kama uti wa mgongo wa usalama wa taifa na kuongeza kuwa itasaidia kupambana na uhalifu wa kiuchumi.
Changamoto za usalama
"Ukosefu wa vitambulisho umekuwa changamoto kubwa sana hata tukizidi kukabiliwa na changamoto nzito za usalama. Hatukuweza kufichua wamiliki wa magari yaliyotumika kwa mashambulizi, washambuliaji wa kujitoa mhanga na utambulisho wa wafadhili wa ugaidi, " Alisema Rais Hassan Sheikh Mohamud.
"Ikiwa mtu mwenye asili ya Kisomali hapo awali alijitambulisha kwa kutumia ukoo, familia yake na jamii, leo anaweza kutambuliwa kibinafsi na kusema kwa kiburi 'mimi Ni Msomali,' Hamza aliongeza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya vitambulisho vya taifa na usajili (NIRA), Abdiweli Ali Timmade, alieleza zoezi la usajili kuwa ni sura mpya katika juhudi za muda mrefu za taifa hilo za kuanzisha vitambulisho.
Waziri wa elimu Farah Sheikh Abdulqadir amesema vitambulisho hivyo vitakuwa muhimu katika sekta ya elimu.
Kadi mpya za utambulisho zimetajwa kuwa na matumaini ya kuleta mchango mkubwa haswa katika sekta za Teknolojia, fedha, anga, uchunguzi wa jinai, kuendesha gari na huduma zingine zinazohitajika na raia wake.