Kufikia mwisho wa Septemba mwaka huu, Wakenya wataweza kupata vitambulisho vipya vya kitaifa vya kidijitali.
Vitambulisho hivi kwa mara ya kwanza vitaweza kutolewa kwa watoto pindi wanapozaliwa pamoja na wengine kulingana na utaratibu uliopo sasa, kama wanaomba kwa mara ya kwanza baada ya kufikisha miaka 18, au waliopoteza vitambulisho vyao.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Uhamiaji na Huduma kwa Raia Julius Bitok, hii itasaidia katika kuimarisha utoaji wa huduma na kujumuishwa kwa raia wote katika mpango wa fedha wa serikali.
''Moja ya faida zake ni, uwepo wa nambari maalum ya usajili, mahususi kwa kila raia,'' amesema Bitok.
Vitambulisho hivyo vya awamu ya tatu vitaigharimu serikali shilingi bilioni moja sawa na dola za kimarekeni milioni 6.8 na inatarajiwa kuichukua serkali muda wa miaka mitatu hadi minne kukamilisha shughuli hiyo ya uhamaji kwa mfumo mpya.
''Kamati ya kitaifa ya usimamizi imeidhinisha kwa ukarimu mapendekezo yaliyotolewa na kamati ya kiufundi ya kitambulisho cha kidijitali ya kutaka utambulisho wa kitaifa wa kidijitali utekelezwe,'' aliongeza Katibu Bitok.
Bora kuliko 'Huduma Number'
Vitambulisho vya Maisha Card vitatumiwa pia katika usajili wa wanafunzi shuleni pamoja na nambari ya usajili wa mitihani ya kitaifa, nambari ya huduma ya afya ya kitaifa, usajili wa hazina ya malipo ya uzeeni na leseni ya uendeshaji wa gari nchini.
Kipengele kingine, kitakachofaidi na vitambulisho vya kidijitali ni usajili ya idadi ya watu ambayo itaunganisha taarifa kwa raia wa Kenya, wahamiaji na wakimbizi.
Katibu huyo alisema kuwa maisha Card itakuwa tofauti na mfumo uliozinduliwa na serikali iliyopita wa 'Huduma Number,' ambao ulizua mtafaruku kutokana na wasiwasi juu ya uhifadhi wa taarifa binafsi na matumizi yake.
Hata hivyo, mahakama nchini humo hatimae iliamuru kusitishwa kwa utumiaji wa mfumo huo wa usajili.
Wakati wa uzinduzi wa jukwaa la e-Citizen mnamo Juni 30, Rais William Ruto aliagiza wizara husika za serikali kuunda kitambulisho cha kidijitali ili kuzingatia viwango vya kimataifa vya hati za usajili.
Wizara ya Uhamiaji sasa itaandaa mikutano ya ushauri na uhamasishaji kote nchini kabla ya uzinduzi wa vitambulisho hivyo Septemba 29.