Rais wa Kenya amesema kuwa kufikia mwisho wa Disemba 2023, azma yake ni kuona hakuna tena hitaji la viza za zusafiri kwa Waafrika kuingia Kenya kwa sababu yoyote.
Rais Ruto amekariri msimamo wake kuwa hii itasaidia kuendeleza biashara na utangamano kwa Waafrika kwa pamoja.
''Nchi 27 barani Ulaya leo zenye zaidi ya watu milioni 430 zimeondoa visa za usafiri kati yao. Bado sisi tunawekeana visa,'' alisema Rais Ruto. 'Naomba niwashawishi kwamba umefika wakati sisi katika bara hili kutambua kwamba kuwa na vizuizi vya visa miongoni mwetu kunatuponda sisi wenyewe,'' aliongeza Rais.
''Wakati watu hawawezi kusafiri, wafanyabiashara hawawezi kusafiri, wawekezaji hawawezi kusafiri, sote tunakuwa tunapoteza kwa jumla,'' alisema Rais Ruto.
Rais wa Kenya pia alielezea kuwa tayari kumekuwa na ukuaji wa zaidi ya 27% kwa uchumi wa Afrika Mashariki hasa kutokana na hatua ya kuondolewa kwa ushuru wa forodha na vizuizi voingine vya usafiri kama adaya viza.
Pia Ruto aliwathibitishia Wakenya kuwa baada ya hatua yake ya mwezi Septemba ya kuondoa viza kwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Rais Felix Tshisekedi pia ametangaza kuwaondolea Wakenya wanaotaka kusafiri huko viza.
Mwezi Oktoba pia Kenya imeondoa viza kwa Raia wa Angola.
Hatua hii ya Kenya imezua masuali miongoni mwa baadhi ya wakenya iwapo mataifa mengine pia yanarudisha hisani hiyo kwa Kenya ?
Hata hivyo wengi wameponmgeza wakisema kuwa ni hatua ya kwanza kwa mwamko mpya wa kuleta umoja wa kikweli kwa bara Afrika.
''Watoto wetu kutoka bara hili wasifungiwe katika mipaka ya Ulaya na pia kufungiwa katika mipaka ya Afrika.'' aliendelea kusema Rais Ruto.
Miongoni mwa nchi zilizoondolewa Visa kusafiri Kenya hivi karibuni ni Afrika Kusini, Angola, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, Congo Brazaville, Eritrea na Comorros.