Wakati ugonjwa wa ajabu ulipoanza kugharimu maisha ya watu katika kijiji kimoja wilayani Bukoba nchini Tanzania, diwani wa eneo hilo, Hamisi Hassan Byeyombo, alichukua jukumu la kuwatahadharisha wakazi wa eneo hilo.
Usiku wa Machi 15, Byeyombo alipewa taarifa kuhusu mtu wa nne katika familia moja kufariki kutokana na ugonjwa usiojulikana. Akiwa msemaji Mkuu wa kata na Mwenyekiti wa maendeleo alijua ni jukumu lake kuchunguza na kuchukua hatua.
Waziri alipotangaza tarehe 21 Machi kwamba ilikuwa Marburg, nilishtuka sana na ikazua tafrani nilipofikiria kuwa ni ugonjwa kutoka mbali au nje huko.
Alikwenda katika Kituo cha Afya cha Mtoma ambako wanafamilia hao walitangazwa kuwa wamefariki. Alipofika akapewa taarifa kuwa kuna mgonjwa mwingine ambaye alikuwa yuko na hali mbaya.
"Niliwapigia simu DMO na Mkurugenzi wa Manispaa saa moja asubuhi ili kuwapa taarifa hizi za watu kufariki kwa njia tatanishi, kwa sababu haya ni maswala ambayo yanawahusu," alisema Byeyombo.
"DMO na RMO walifika asubuhi iliyofuata kuchukua sampuli za kuchunguza na kujadili taratibu za mazishi ya wale waliofariki."
RMO akatuma sampuli za kliniki za reverse transcription-polymerase chain reaction (RT-PCR) kwa Maabara ya Kitaifa Dar-es-Salaam.
Marburg Tanzania
Mnamo Machi 21, 2023, Wizara ya Afya ya Tanzania ilitangaza mlipuko wa Ugonjwa wa Virusi vya Marburg (MVD) nchini.
Inaambukizwa kwa watu kutoka kwa popo na wanyama pori na kisha huenea kwa kugusa maji ya mwili ya watu walioambukizwa.
Dalili hizo ni pamoja na homa kali, maumivu makali ya kichwa hutokea ndani ya siku saba baada ya kuambukizwa, kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni(WHO).
Mlipuko wa Tanzania ulikuja mwezi mmoja baada ya Equatorial Guinea kuthibitisha mlipuko wake wa kwanza wa ugonjwa wa virusi vya Marburg pia.Nchi zote mbili zimethibitisha jumla ya kesi 21.
Kupona kwa shida
Mwanaume huyo ambaye Diwani Byeyombe alikuta usiku huo akivuta pumzi za mwisho katika Kituo cha Afya cha Mtoma alikua anaitwa Mushobozi Washington.
Byeyombe alipanga mara moja uhamisho wake ili apelekwe kituo cha karantini wilaya hiyo hiyo ya Bukoba.
Washington ni msaliaji wa MVD; aliipata Februari 28, baada ya kumsindikiza mvuvi mwenzake hospitalini.
“Nimesikia kuwa huyo mwanaume ametoka kwenye harusi hivyo nilifikiri kuna mtu amempiga nilipoona macho yake mekundu na akikohoa damu.Tukiwa njiani kuelekea hospitalini nilitumia kitambaa kumpanguza usoni bila kujua ni ugonjwa gani.” Washington aliiambia TRT Afrika.
Siku chache baada ya kumsaidia rafiki yake, Washington alianza kuhisi uchovu, kwa hiyo akaenda kwenye duka la dawa ili kupata dawa za kupunguza maumivu. Alipimwa malaria japo haikupatikana. Siku tano baadaye hali yake ilizidi kuwa mbaya kwani alianza kutapika kila baada ya saa mbili hadi tatu.
“Ninaishi na mke wangu na wanafamilia wengine wawili, hali yangu ilipoanza kuwa mbaya, niliwaambia nahitaji kwenda hospitalini, wakanipeleka. Mama yangu ambaye anaishi nasi, aliugua muda mfupi baada ya hapo.” Washington alisema.
Washington alilazwa katika Kituo cha Afya cha Mtoma kwa wiki moja, akiendelea kutapika mara kwa mara huku akilishwa kwa njia ya mrija wa vena.
“Niliambiwa mama yangu ni mgonjwa sana. Niliwaomba watu wa pale hospitali waniruhusu niondoke niende kumuuguza mama yangu. Nilipofika nyumbani niliambiwa alipelekwa hospitali kwa hio nikabaki nyumbani, sikuwa na nguvu" Alieza Washington nakuongeza "hadi nikaanza kukohoa damu”.
Kwa sasa hakuna matibabu au chanjo mahususi ya virusi vya Marburg, na ugonjwa huo unadhibitiwa kupitia huduma ya usaidizi, kama vile maji na ugiligili kuongezwa mwilini na matibabu ya maambukizo yoyote yale husika.
Serikali ya Tanzania ilitangaza wiki iliyopita kuwa nchi hiyo haina Marburg na iko wazi kwa wageni. Kituo cha karantini kimefungwa hivi karibuni pia.
Walakini, kulingana na Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa,ingawa Marburg inachukuliwa kuwa "ugonjwa adimu sana kwa watu", inapotokea, ina uwezo wa kuenea" na inaweza kusababisha kifo.