China imetangaza mpango wa kuimarisha ushirikiano wa kijeshi na nchi za Afrika, hatua ambayo itaimarisha zaidi msimamo wake wa kuwa miongoni mwa washirika wakuu wa kibiashara na maendeleo wa bara hilo.
Akizungumza wakati wa Kongamano la tatu la Amani na Usalama la China na Afrika mjini Beijing, Waziri wa Ulinzi Li Shangfu alisema ushirikiano wa China na Afrika utaimarisha usalama na utulivu wa kimataifa.
"Katika siku zijazo, China itaimarisha ushirikiano wa kijeshi na Afrika katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na mazoezi ya pamoja, ulinzi wa amani na kusindikiza, elimu ya kijeshi pamoja na mafunzo ya kitaaluma ili kuongeza uhakika zaidi, utulivu na nishati chanya kwa dunia yenye misukosuko," Li aliambia kongamano.
Wawakilishi kutoka karibu nchi 50 na mashirika ya kikanda barani Afrika wanahudhuria kongamano hilo la siku sita wiki hii.
“China ni nchi kubwa zaidi inayoendelea na Afrika ndilo bara lenye nchi zinazoendelea zaidi. China na Afrika zinashiriki utajiri na malengo. China inapenda kusimama kidete na watu wa Afrika kutekeleza Mpango wa Usalama wa Dunia na kujenga jumuiya ya China na Afrika yenye mustakabali wa pamoja," Li alisema.
Mwaka 2022, uwekezaji wa moja kwa moja wa China barani Afrika ulikuwa dola bilioni 3.4. Ni chanzo cha nne kwa ukubwa cha uwekezaji barani Afrika, na kuna zaidi ya kampuni 3,000 za China katika bara hilo, kulingana na Wizara ya Biashara.
Mpango wa Usalama wa Kimataifa ulipendekezwa na Rais wa China Xi Jinping mwaka jana mwezi Aprili.
"Inalenga kuondoa sababu kuu za migogoro ya kimataifa, kuboresha utawala wa usalama wa kimataifa, kuhimiza juhudi za pamoja za kimataifa za kuleta utulivu na uhakika zaidi katika enzi tete na inayobadilika, na kukuza amani na maendeleo ya kudumu duniani." Li aliongeza.