Kumekuwa na mjadala katika bunge ya taifa la Uganda kuhusu sababu za Rais Yoweri Museveni kutohudhuria mikutano ya kimataifa.
Ssemujju Nganda mbunge wa Manispaa ya Kira amesisitiza haja ya Bunge kuangalia afya ya Rais Yoweri Museveni kufuatia kushindwa kuhudhuria mikutano muhimu ya kimataifa ambayo amekuwa akihudhuria siku za nyuma.
Hii ilifuatia maelezo ya Spika wa Bunge kuwa Uganda inawakilishwa na Makamu wa Rais, Jessica Alupo huko Samoa katika Mkutano wa Jumuiya ya nchi za Madola CHOGM.
“Tulikuwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hivi karibuni, na Rais aliwakilishwa na Makamu wa Rais, tulikuwa na mkutano Uchina, na tena, Rais wetu aliwakilishwa, na umesema hivi punde hata kwa Jumuiya ya Madola," Nganda alisema bungeni.
"Naomba kuuliza, Bunge hili linaweza kuwa halijazingatia umuhimu wa kuangalia afya ya Rais wetu kutokana na umri wake. Mikutano hii yote muhimu ambayo amekuwa akihudhuria kitamaduni, sasa hawezi kuhudhuria," aliongezea.
Hata hivyo, Spika wa Bunge Anita Among amesema haoni uzito wa Rais kutohudhuria mikutano binafsi.
Alishangaa ni kwa nini hilo limezua mjadala kuhusu afya ya Rais Museveni, akisema uamuzi wake wa kuwateua maafisa wengine unatokana na fursa ya kuwa na Naibu, kama vile vile yeye alivyo na Naibu Spika Thomas Tayebwa, ambaye ni mwenyekiti wa vikao pia.
“Hiyo ndiyo faida ya kuwa na Naibu, kwa nini usilalamike wakati Naibu wangu anaongoza hapa? Unafaa kumpa fursa Naibu wako na nijuavyo Rais Museveni anaweza kuwa na afya bora kuliko baadhi yetu. Tulipitisha Sheria hapa kwamba tunaweza kushiriki mitandaoni pia na nimemwona Janet Kataha ( mke wa rais na Waziri wa Elimu) mtandaoni kila wakati, hata sasa, yuko mtandaoni ikiwa ungependa kuona. Ikiwa tuna masuala ya elimu, atatushughulikia kuhusu elimu,” alisema Spika.
Wakati huo huo, Spika wa Bunge Anita Among amekanusha taarifa kwamba amezuiwa kuingia Samoa kuiwakilisha Uganda kwenye Mkutano wa Wakuu wa Serikali za Jumuiya ya Madola (CHOGM) unaoendelea.
"Mkutano wa CHOGM ulifunguliwa Samoa jana na kama Uganda, hakuna tamko lolote linalotolewa kuhusu ushiriki wetu kama nchi. Tunasoma taarifa kuhusu wewe kusimamishwa kuhudhuria CHOGM lakini sisi ni Bunge la Uganda. Je, hiyo pia inazuia Bunge la Uganda kushiriki katika Jumuiya ya Madola?" aliuliza Theodore Ssekikubo mbunge wa kaunti ya Lwemiyaga.
Lakini Spika Among amejitetea kuwa anatarajiwa kusafiri kuelekea India jioni ya leo, kuhudhuria Mkutano wa Maspika na Maafisa Wasimamizi wa Jumuiya ya Madola.
"Nimesimamishwa kuhudhuria mkutano gani wa Jumuiya ya Madola? Kwa kweli ninaenda kwenye mkutano wa Jumuiya ya Madola usiku wa leo. Mimi ni mwenyekiti wa Maspika wa Jumuiya ya Madola, mkutano wetu ujao tunaufanyia India. Kwa hiyo, ile ya Samoa inahudhuriwa na Makamu wa Rais, Jessica Alupo, akimwakilisha Rais," Spika alielezea.