Mmoja wa waandamanaji akiwa amebeba Siwa iliyodaiwa kuibiwa ndani ya Ukumbi wa Bunge, jijini Nairobi siku ya Juni 25, 2024./Picha: Wengine

Bunge la Kitaifa nchini Kenya limekana taarifa za kuibiwa kwa Siwa ndani ya Bunge hilo wakati wa maandamano ya Juni 25, 2024.

Hii inafuatia kusambaaa kwa picha video zinazoonesha waandamanaji wakiwa wamebeba fimbo hiyo yenye kuwakilisha mamlaka ndani ya Ukumbi wa Bunge katika nchi za Jumuiya ya Madola.

Badala yake, ofisi ya bunge la Kenya imesisitiza kuwa kilichokuwa kinazungushwa na waandamanaji ni mfano tu wa Siwa hiyo iliyokuwa imewekwa ndani ya ukumbi wa Bunge hilo jijini Nairobi, na kuongeza kuwa Siwa hiyo bado iko salama mahali pake.

Mbali na Siwa, baadhi ya waandamanaji hao walionekana wakiwa wamevaa mavazi yanayovaliwa na wapambe wa Bunge wakati wa vikao na mijadala.

Siwa ni nini?

Matumizi ya kifaa hichi yalianza karne 18, wakati duniani inashuhudia Mapinduzi makubwa ya viwanda ya nchini Uingereza.

Kulingana na Charles Kadonya, ambaye pia ni Katibu katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA), matumizi ya Siwa yamekuwa ya kawaida sana katika nchi wanachama wa Jumuiya za Madola.

Matumizi ya kifaa hicho yalianzia nchini Uingereza wakati wa mapinduzi ya viwanda vya Uingereza wakati wa karne ya 18./Picha: Wengine

"Fimbo hii huwakilisha mamlaka na ukweli ni kwamba, hakuna kikao chochote kinachoweza kufanyika au shughuli rasmi yoyote ile bila uwepo wa fimbo au chuma hiki," Kadonya anaiambia TRT Afrika.

Wakati huo, wananchi wa Uingereza walitaka wawe na alama ya mamlaka, hususani wanapojadili mambo yanahusu mustakabali wao.

"Na ndio maana wakaamua kuja na fimbo maalumu itakayoashiria uwepo wa mamlaka na nguvu wakati wa majadiliano yao," anaongeza.

Kwa mujibu wa Kadonya, kifaa hiki hubebwa na wapambe wa Bunge, wanaojulikana kama 'Sergeant At Arms', na huhifadhiwa kwenye sehemu yenye usalama.

Fimbo hii huwakilisha mamlaka na ukweli ni kwamba, hakuna kikao chochote kinachoweza kufanyika au shughuli rasmi yoyote ile bila uwepo wa fimbo au chuma hiki./Picha: Bunge TZ X

Kulingana na Kadonya, fimbo hiyo hubebwa na mpambe wa Bunge akimtangulia Spika, Naibu Spika au Mwenyekiti wakati anapoingia na kutoka kwenye ukumbi wa bunge, huku watu wote wakiwa kimya.

Siwa hutengenezwa kwa kutumia vitu mbalimbali iwemo mbao na hata madini kama vile dhahabu na shaba na hufikia uzito wa kilogramu 10, huku gharama zake zikifikia hadi dola za Kimarekani milioni 1.

Siwa ikiwa mbele ya kiti cha spika wakati wa mjadala ndani ya Bunge la EALA./Picha: EALA X
TRT Afrika