Senegal inapaswa kufanya uchaguzi wa rais haraka iwezekanavyo, Umoja wa Afrika (AU) ulisema, siku chache baada ya Rais wake Macky Sall kuchelewesha kura ya Februari 25 hadi tarehe ambayo haikutajwa.
Mwenyekiti wa Tume ya AU Moussa Faki Mahamat alisema katika taarifa yake Jumapili jioni kwamba Senegal inapaswa "kuandaa uchaguzi haraka iwezekanavyo, kwa uwazi, amani na utangamano wa kitaifa".
“AU Inahimiza nguvu zote za kisiasa na kijamii kutatua mzozo wowote wa kisiasa kupitia mashauriano ya kistaarabu, kuelewana na mazungumzo...,” iliongeza taarifa hiyo.
Wabunge wa Senegal wanatakiwa kujadiliana siku ya Jumatatu kuhusu pendekezo la kufanyika kwa kura Agosti 25 na kumweka Sall madarakani hadi mrithi wake atakapoteuliwa, kulingana na maandishi ya mswada ulioonekana na Reuters.
Vikosi vya usalama vya Senegal vimetawanya umati wa watu waliokuwa wamekusanyika katika mji mkuu wa Dakar siku ya Jumapili kupinga kuahirishwa kwa uchaguzi wa rais wa Februari 25.
Rais Macky Sall alitangaza Jumamosi kuwa kura hiyo itacheleweshwa hadi tarehe ambayo haijatajwa kutokana na mzozo kuhusu orodha ya wagombea - hatua iliyokataliwa na vyama vya upinzani.
Pia ripoti ziliibuka Jumapili za kukamatwa kwa kiongozi wa upinzani, ambaye ni Waziri mkuu wa zamani wa Senegal Aminata Toure.
Senegal haijawahi kuchelewesha uchaguzi wa rais, na tangazo la Sall siku ya Jumamosi liliiweka nchi katika hali ya kikatiba isiyojulikana ambayo baadhi ya vyama vya upinzani na mashirika ya kiraia yalisema ni sawa na "mapinduzi ya kitaasisi".