Coletta Wanjohi
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Kampeni za kusaka nafasi ya juu ya uongozi wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) inaendelea kunoga ambapo wagombea kutoka nchi tatu za eneo la Afrika mashariki, wameonesha nia ya kugombea, ikiwemo Somalia.
AUC ni Sekretarieti ya Umoja wa Afrika ambayo shughuli zake zimejikita zaidi katika utendaji. Jukumu lake kuu ni kufuatilia utekelezaji wa maamuzi ya viongozi wa nchi za Afrika.
Kwa maani hiyo, Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika yuko chini ya Umoja wa Afrika ambayo ni umoja wa nchi 55 za AU.
Nafasi hiyo kwa sasa inashikiliwa na aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Chad Moussa Faki Mahamat.
Somalia inaendelea kumpigia debe Fawzia Yusuf Haji Adam aliyeteuliwa na nchi hiyo Januari 2024 kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika. Fawzia Yusuf Haji Adam ni mwanasiasa wa Somalia.
Aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Naibu Waziri Mkuu wa Somalia kati ya Novemba 2012 hadi Januari 2014.
Mwanadiplomasia huyo aliwahi kuhudumu kwneye ubalozi wa Somalia huko Moscow, Washington DC, Berlin na Paris, akifanya kazi katika serikali ya Somalia na Umoja wa Mataifa. Pia aliwahi kugombea urais mwaka 2022.
Kwa sasa anaongoza Chama cha National Democratic Alliance (NDA) nchini Somalia na anahudumu kama mbunge wa shirikisho. Kwa sasa anasomea sera ya Kimataifa ya Umma katika Chuo cha Mafunzo ya Kimataifa ya Chuo Kikuu cha John Hopkins.
Iwapo atanyakua nafasi hiyo, Fawzia atakuwa mwanamke wa pili kuongoza Tume hiyo, baada ya Nkosazana Dlamini-Zuma wa Afrika Kusini aliyeongoza tume hiyo kati ya 2012 na 2017.
Chini ya utaratibu uliowekwa wa mzunguko wa mwaka wa 2018, eneo la Afrika Mashariki linapaswa kutoa Mwenyekiti wa AUC.
Kanuni za uchaguzi zinaruhusu wagombea wengi kutoka eneo hilo, na hivyo kuchochea ushindani wa mara moja kwa uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Februari 2025.
Fawzia Yusuf Haji Adam anagomba nafasi hii ambayo pia inawaniwa na alityekuwa waziri mkuu wa Kenya Raila Odinga na waziri wa mambo ya nje wa Djibouti Mahmoud Youssou.
Kwa sasa, Somalia ina imani kubwa katika kiti hiki hasa baada ya OIC, yenye takribani mataifa 30 ya Afrika kama wanachama wa Afrika kutangaza kuwa itaunga mkono Somalia kwa nafasi ya mwenyekiti wa AUC kwa muhula wa 2025-2028.