katika msimu wa mvua kati ya Aprili na Juni mwaka huu, mvua iliyonyesha Afrika Mashariki ilipindukia matarajio na kusababisha maafa kutokana na mafuriko/ Picha : TRT Afrika

Kituo cha Afrika cha ufuatiliaji wa Hali ya Hewa kwa Maendeleo barani Afrika ACMAD, kimetoa tahadhari ya mvua kubwa na mafuriko kunyesha katika nchi nyingi za Afrika ya Mashariki na Kati na uwezekano wa kusababisha maafa makubwa.

Shirika hilo la ACMAD limeonya kuwa mataifa takriban 12 katika kanda hiyo nzima yana uwezekano wa kupokea mvua kwa wingi wa zaidi ya milimita 100-150 kati ya Novemba 22 had 27.

Kwa mujibu wa taarifa yao waliochapisha katika mtandao wa X, nchi zitakazoathirika ni pamoja na Rwanda, Burundi, Gabon, Congo,Angola Uganda, Kenya, Tanzania, Zambia, Ethiopia, Malawi na Madagascar.

Athari ya mvua hii

Kwa mujibu wa tahadhari waliyotoa, kuna hatari kubwa ya watu wengi kuachwa bila makao kufuatia mafuriko na nyumba zao kusombwa, mlipuko wa magonjwa yanayosambazwa na maji machafu na kusombwa au kuharibiwa kwa miundo mbinu kama barabara na madaraja.

ACMAD pia imeonya kutokea maporomoko ya ardhi katika baadhi ya maeneo hasa nchi zilizo na milima.

Japo huu ni msimu wa mvua eneo la Afrika Mashariki, na tayari baridi, kali, mvua na utanda wa mawingu unafanyika katika maeneo mengi. Wengi wanahofia kwani katika miaka ya hivi karibuni misimu ya hali ya anga imevurugika kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.

katika msimu wa mvua kati ya Aprili na Juni mwaka huu, mvua iliyonyesha Afrika Mashariki ilipindukia matarajio na kusababisha maafa kutokana na mafuriko.

Nchini Kenya: Mto Nairobi na Mto Athi zote zilipasua kingo zake na kuwafanya watu 40,000 kuyahama makazi. Takriban vifo 300 viliripotiwa. Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu pia iliripoti angalau mifugo 960 na ekari elfu 24 za mashamba zilifurika.

Shule nchini Kenya pia zililazimishwa kufungwa hadi hali ilipotangamaa baadaye.

Nchini Tanzania: Mto Rufiji Kaskazini mwa Tanzania ulivunja Kingo zake na kusababisha mojawapo ya mafuriko mabaya zaidi kuwahi kutokea. Kufikia Aprili mwaka huu mafuriko kaskazini mwa Tanzania yaliua watu 161, kujeruhi wengine 250, kuharibu zaidi ya nyumba 10,000 na kuathiri watu 210,000 katika kaya 51,000.

Wataalamu wa hali ya hewa wanashauri serikali na mamlaka husika kuchukua hatua za tahadhari kama kuwahamisha watu inapohitajika, kudhibiti maji ya mabwawa na kujiandaa kuchukua hatua za dharura inapotokea ripoti za mwanzo za mafuriko katika maeneo yao.

TRT Afrika