Uturuki imelaani vikali mauaji yaliyosababishwa na jeshi la Israeli dhidi ya Wapalestina waliokosa makazi katika kambi iliyoko katika shule ya Tabaeen katikati mwa Gaza.
"Israeli imetekeleza aina mpya ya uhalifu dhidi ya binadamu kwa kuua zaidi ya raia mia moja walikuwa wamejihifadhi katika jengo la shule katika eneo la Daraj lililopo mjini Gaza," Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki ilisema katika taarifa yake siku ya Jumamosi.
Wizara hiyo iliilaani serikali ya Netanyahu ikisema: "Kwa mara nyingine tena, tukio hili linadhirisha namna serikali ya Netanyahu ilivyokusudia kuhujumu mchakato wa kumaliza vita."
Taarifa hiyo pia inasisitiza kwamba wahusika wa kimataifa ambao hawachukui hatua dhidi ya hatua za Israeli wanashiriki katika uhalifu huu.
Mabomu makubwa matatu
Siku ya Jumamosi, Mkurugenzi wa ofisi ya habari mjini Gaza alisema kuwa ndege ya Israeli iliilenga kwa mabomu makubwa matatu, shule ya Tabaeen inayohifadhi zaidi ya watu 6,000 wasio na makazi.
Kulingana na Ismail Thawabteh, ndege za Israeli zilidondosha mabomu matatu, yenye uzito wa zaidi ya kilo 900, kila moja.
Shambulizi hilo lilisababisha vifo ya watu zaidi ya 100, wengi wakijeruhiwa na kupoteza viungo muhimu mwilini.