Erdogan ametoa rai kwa jumuiya ya kimataifa kuchangia katika amani na haki ulimwenguni kwa kuunga mkono hadhi ya dola ya Kipalestina./Picha: AA  

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameweka msisitizo kwenye umuhimu wa kuishirikisha Uturuki katika juhudi za ulinzi za Umoja wa Ulaya, pia akionesha umuhimu wa kudumisha amani na usalama wa bara la Ulaya.

Rais Erdogan ametoa kauli hiyo siku ya Alhamisi, wakati wa ziara yake jijini Budapest kuhudhuria Mkutano wa Kisiasa wa Jumuiya ya Ulaya, ambapo pia alikosoa ucheleweshwaji wa mchakato wa kuiingiza Uturuki kwenye umoja huo.

“Hakuna sababu yoyote inayoeleweka ya kuizuia nchi kama Uturuki kuingia kwenye umoja huo, ikizingatiwa inachangia kwa kiasi kikubwa kwenye usalama na mafanikio ya bara la Ulaya.”

Vilevile, Erdogan aligusia umuhimu wa hatua za pamoja za kukabiliana na ugaidi, akitaka nchi washirika wa Ulaya kuonesha ushirikiano katika mapambano dhidi ya PKK.

Pia aligusia ushirikiano wa kimahakama na kiutawala baina ya nchi za Ulaya, ambapo FETO bado iko hai.

Juhudi za kuunda nafasi ya kidiplomasia

Akizungumzia mgogoro unaendelea wa Ukraine, Erdogan alionya kuhusu kuongeze kwa athari zake na kupungua kwa nafasi za kidiplomasia.

"Matokeo mabaya ya vita nchini Ukraine yanazidi kuongezeka kila siku, na kuacha nafasi ndogo ya diplomasia," alisema. Erdogan aliangazia mikutano yake ya hivi karibuni na Rais wa Urusi Vladimir Putin na maafisa wa Ukraine, akisisitiza wito wake wa kuunda nafasi ya diplomasia.

Rais huyo pia alilaani mauaji ya kimbari ya Israeli huko Gaza, na kuyataja ''aibu ya pamoja kwa ubinadamu''. Akirejea mzozo unaoendelea ambao umesababisha vifo vya karibu watu 50,000, Erdogan alisisitiza hitaji la dharura la kusitishwa kwa mapigano na kuongezeka kwa misaada ya kibinadamu.

Erdogan aliongeza: "Shinikizo kwa Israeli ni la muhimu ili kuhakikisha usitishaji wa mapigano na uwasilishaji wa misaada ya kibinadamu ya kutosha katika eneo hilo.

"Wale wanaounga mkono bila masharti uvamizi wa Israel lazima wajue wanahusika katika uhalifu huu," alisisitiza.

Ametoa wito kwa nchi ambazo bado hazijaitambua Palestina kufanya hivyo, na kuitaka jumuiya ya kimataifa kuchangia haki na amani duniani kwa kuunga mkono utawala wa Palestina.

Atarajia hatua kutoka kwa nchi wanachama

Kando ya mkutano huo, Erdogan pia alikutana na viongozi mbalimbali akiwemo Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Waziri Mkuu wa Uholanzi Dick Schoof, Waziri Mkuu wa Denmark Mette Frederiksen, na Rais wa Kamisheni ya Ulaya Ursula Von der Leyen.

Rais Erdogan alisisitiza kuwa Uturuki inatarajia kuona hatua kutoka kwa nchi wanachama kufufua mchakato wake wa kujiunga na Umoja wa Ulaya na kuimarisha Umoja wa Forodha, ambao utasababisha kuwezesha EU.

Viongozi hao, pia walijadiliana masuala ya kikanda na ya kiulimwengu.

Viongozi wa Ulaya wamekutana Budapest kwenye mkutano wa tano wa Kisiasa wa Jumuiya ya Ulaya (EPC), ambapo walijadiliana masuala mbalimbali ya ulimwenguni likiwemo suala la Ukraine na Mashariki ya Kati.

Waziri Mkuu wa Hungari Viktor Orban ndiye alikuwa mwenyeji wa mkutano huo, ambapo pia uliangazia masuala ya uhamiaji na usalama wa kiuchumi barani Ulaya.

TRT Afrika