Erdogan alisema Uturuki hadi sasa imetuma zaidi ya tani 84,000 za misaada huko Gaza, na iko tayari kutuma mengi zaidi vikwazo vitakapoondolewa. / Picha: AA

Rais wa Uturuki amekosoa kutokuwa na mwitikio wa nchi za Kiislamu katika kushughulikia mauaji ya halaiki yanayoendelea Gaza, huku akiyashutumu mataifa ya Magharibi kwa kutoa uungaji mkono kamili kwa Israeli.

"Nchi chache za Magharibi zimetoa kila aina ya msaada kwa Israeli, wakati nchi za Kiislamu zimeshindwa kujibu ipasavyo kumesababisha hali kufikia hatua hii," Recep Tayyip Erdogan alisema Jumatatu katika Mkutano wa Pamoja wa Ushirikiano wa nchi za Kiislamu na Jumuia ya nchi za Kiarabu unaofanyika mji wa mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh.

Erdogan alisema Uturuki hadi sasa imetuma zaidi ya tani 84,000 za misaada huko Gaza, na iko tayari kutuma mengi zaidi vikwazo vitakapoondolewa.

Israel haiwezi hata kuvumilia uwasilishaji wa misaada ya kibinadamu huko Gaza na imekuwa ikihifadhi vifaa vya msaada nchini Misri kwa miezi kadhaa, Erdogan alisema zaidi.

"Tuko tayari" kutekeleza hatua zote zinazoonekana ambazo zitaonyesha gharama kubwa ya kuendelea kwa serikali ya Netanyahu kukalia kwa mabavu ardhi ya Palestina, rais wa Uturuki alisema.

"Tunapaswa kuhimiza nchi nyingi iwezekanavyo kujiunga na kesi iliyowasilishwa na Afrika Kusini dhidi ya Israeli katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki," alisisitiza.

Mvutano wa kieneo umeongezeka kutokana na mashambulizi ya kikatili ya Israeli dhidi ya Gaza, ambayo yameua zaidi ya watu 43,600, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, kufuatia shambulio la kundi la Hamas la Palestina mwaka jana.

Huku mzozo huo ukienea hadi Lebanon, Israeli imeanzisha mashambulizi mabaya kote nchini, karibu watu 3,200 wameuawa na wengine zaidi ya 13,800 kujeruhiwa katika mashambulizi hayo tangu mwaka jana, kwa mujibu wa mamlaka ya afya ya Lebanon.

Licha ya onyo la kimataifa kwamba eneo la Mashariki ya Kati liko kwenye hatari ya kuzuka kwa vita vya kikanda, Tel Aviv ilipanua mzozo huo kwa kuanzisha uvamizi wa ardhini mnamo Oktoba 1 kusini mwa Lebanon.

TRT World