Hatimaye Israel italipa gharama ya mauaji ya halaiki ambayo yamekuwa yakiendelea huko Gaza kwa mwaka mmoja, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema.
Alisisitiza kuwa makumi ya maelfu ya watu, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wameuawa huko Gaza katika mwaka mmoja, na taasisi nyingi huko Gaza, pamoja na hospitali na shule, ziliharibiwa.
"Kama Uturuki, tutaendelea kusimama dhidi ya serikali ya Israeli, bila kujali litakalotokea, na kutoa wito kwa ulimwengu kujiunga na msimamo huu wa heshima," Erdogan aliongeza.
Israeli imeendeleza vita vyake dhidi ya Gaza kufuatia shambulio la kundi la wapiganaji wa Palestina Hamas Oktoba mwaka jana, licha ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutaka kusitishwa mara moja kwa mapigano.
Tangu wakati huo, karibu watu 42,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wameuawa, na zaidi ya wengine 97,100 wamejeruhiwa, kulingana na mamlaka ya afya ya eneo hilo.
Mashambulizi yanayoendelea ya Israeli yamewafanya takriban wakazi wote wa Gaza kuyahama makazi yao, na hivyo kuzidisha uhaba wa chakula, maji safi na dawa kutokana na kuzingirwa kwa muda mrefu.
Israel kwa sasa inakabiliwa na mashtaka ya mauaji ya halaiki katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki kufuatia uhalifu wake huko Gaza.