Hii ndiyo mara ya kwanza kwa Kipyegon kushindwa katika mbio za umbali wowote msimu huu./ Picha : X- WRRC Riga

Na Lynne Wachira

TRT Afrika, Nairobi, Kenya

Medali saba za dhahabu kati ya nane ambazo zilikuwa zinashindaniwa katika Makala ya kwanza kabisa ya mashindano ya dunia ya kukimbia barabarani zimewaendea wanariadha kutoka mataifa ya Afrika mashariki haswa Kenya na Ethiopia.

Diribe Welteji kutoka Ethiopia aling'aa zaidi ya wote kufuatia ushindi wake katika mbio za umbali wa maili moja upande wa wanawake na kuandikisha rekodi mpya ya dunia ya muda wa 4:21:00.

Wengi walimpigia upato mshikiliaji wa rekodi ya dunia ya mbio za mita 1500 Faith Kipyegon kuibuka mshindi kwa urahisi kwani amemaliza katika nafasi ya kwanza katika mbio zote ambazo ameshiriki mwaka huu.

Kipyegon alianza vilivyo na kwa kasi ya juu ishara tosha kuwa alitaka kumaliza msimu mwaka huu kwa ushindi.

Hata hivyo Welteji aliongeza kasi huku Faith akionekana kufifia na hatimaye kumaliza katika nafasi ya tatu nyuma ya Freweyni Hailu ambaye alihakikishia Ethiopia nafasi mbili za kwanza.

Hii ndiyo mara ya kwanza kwa Kipyegon kushindwa katika mbio za umbali wowote msimu huu.

Historia kwa Mkenya Peres Jepchirchir katika Half Marathon

Mkenya Peres Jepchirchir aliliorodhesha jina lake kwenye kitabu cha historia alipoibuka bingwa wa dunia wa mbio za half marathon kwa mara ya tatu.

 Jepchirchir ni miongoni mwa wanaridha wa pekee wa kike ambao ni bingwa mara tatu wa mashindano ya Dunia ya half marathon./ Picha : X-  WRRC Riga 23

Jepchirchir alikabiliana na ushindani mkali kutoka kwa mkenya mwenzake Margaret Chelimo na akanyakua ushindi akitumia muda wa 1:07:25 ambao ni rekodi mpya ya mashindano hayo.

Aliandikisha ushindi katika Makala ya mwaka wa 2016 na 2021, mafanikio katika Makala ya mwaka huu ni ya kipekee kwani anajiunga na wanaridha tajika kama vile Tegla Lorupe (Kenya), Lorna Kiplagat ( Netherlands) na Paula Radcliffe (Uingereza) kama wanaridha pekee ambao ni bingwa mara tatu wa mashindano ya Dunia ya half marathon.

Kenya ilinyakua medali zote katika kitengo hiki huku Margaret Chelimo na Catherine Amanang’ole wakimaliza katika nafasi ya pili na ya tatu mtawalia.

Vile vile, hii ni mara ya tatu kwa Kenya kuzishinda medali zote katika kitengo hiki baada ya Makala ya 2014 na Makala ya 2016 ambayo pia Peres Jepchirchir alinyakua dhahabu.

Tatu Bora kwa Kenya katika Kitengo cha Half Marathon - wanaume

Mashabiki wa riadha wa Kenya hawakusitisha sherehe kwani walijikuta katika hali ya ushindi mkubwa kwa mara nyingine takriban saa moja tu baada ya ushindi mkubwa wa wanawake.

Takriban wanariadha mia nne kutoka mataifa 57 na vile vile timu ya wakimbizi walishiriki mashindano hayo ya siku moja./ Picha X - World Athletics

Baada ya washiriki kusalia kwa pamoja kwa muda Sebastien Sawe na Daniel Ebenyo walionyesha nia ya kutwaa ubingwa huku Sawe akimpiku mshindi huyo wa nishani ya fedha katika mbio za mita 5000 na kuishindia Kenya dhahabu ya tatu katika mashindano hayo.

Daniel Ebenyo alilazimika kuridhika na fedha huku Samwel Mailu akikamilisha orodha ya tatu bora.

Bingwa wa Jumuiya ya Madola ndiye bingwa wa dunia wa mbio za barabara.

Hapo awali bingwa wa Jumuiya ya madola katika mbio za mita 5000, Beatrice Chebet alionyesha ueledi wake katika viwanja tofauti na kushinda dhahabu ya kwanza ya mashindano ya dunia ya barabara, ikiwa ni katika mbio za kilomita tano.

Alitumia muda wa dakika 14:35 mbele ya mkenya Lilian Kasait huku Ejgayehu Tawe kutoka Ethiopia akihakikisha kuwa medali zote zitasafiri kutoka bara Ulaya hadi Mashariki mwa Afrika.

Beatrice Chebet alifungua msimu wa mwaka huu kwa ushindi na akaufunga vivyo hivyo, Mapema mwaka huu, aliibuka bingwa wa dunia wa mbio za nyika ambazo zilifanyika mjini Bathurst Australia.

Katika mbio za kilomita tano upande wa wanaume, Hagos Gebrhiwet wa Ethiopia aliibuka mshindi mbele ya mwananchi mwenza Yomif Kejelcha huku Nicholas Kimeli wa Kenya akiwa katika nafasi ya tatu.

Takriban wanariadha mia nne kutoka mataifa 57 na vile vile timu ya wakimbizi walishiriki mashindano hayo ya siku moja.

Medals Table marathon
TRT Afrika