Nyota Chipukizi wa Kenya Davis Agesa, Maarufu kama 'Davis' alisimulia kuangukia mtego wa wakala bandia baada ya kutambulishwa kwa wakala huyo na mtu wa karibu aliyemwamini.
Kuahidiwa kuchezea klabu ya daraja la juu nchini Malaysia, pamoja na ada ya kusajiliwa, mshahara mnene, na faida nyingi, ilionekana kama fursa ya aina yake kwa Davis.
"Niliunganishwa na wakala huyo na mtu wangu wa karibu niliyemuamini sana. Kwa hivyo, nilipopata mwaliko kwamba nitaweza kuichezea kilabu ya kiwango cha Juu nchini Malaysia, sikuwa na mashaka yoyote, " Davis alisimulia.
Davis alianza kujiandaa kwa safari yake, ikiwa ni pamoja na kununua tiketi yake ya ndege kuelekea Malaysia iliyomgharimu takriban dola 600 za kimarekani, mara tu kile kilichoonekana kuwa hati halali zilizoelezea masharti ya makubaliano hayo zilipotolewa.
"Tulidumisha mawasiliano yetu na wakala huyo ambaye kila mara alinihakikishia kuwa kila kitu kilikuwa kikienda shwari na klabu hiyo ambayo ingenisajili. Kwa hakika sikuwa na mawazo mengi ya kutiliwa shaka kwa sababu nilikuwa nimeunganishwa na wakala huyu na mtu wa karibu sana katika taaluma yangu ya mpira wa miguu, " aliongeza.
Ghafla mchana uligueka usiku kwa Davis pindi alipofika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kuala Lumpur.
Hii ni kwa kuwa, Davis hakukutana na mtu yeyote katika uwanja wa ndege kinyume na matarajio yake kwani hakuna aliyekuwepo kumkaribisha kama alivyoahidiwa.
"Pindi tu baada ya kutua kwenye uwanja wa ndege ndipo nilipoanza kuhisi kuwa hali haikuwa sawa. Kwa kawaida ungetarajia mtu akupokee kutoka uwanja wa ndege hadi mahali unapoishi, lakini haikuwa hivyo, " alisimulia.
Jitihada za Davis za kuwasiliana na wakala huyo bandia ziliambulia patupu, na Davis alijikuta akihangaika katika uwanja wa ndege wa Kuala Lampur, huku akiogopa kukubali ukweli kwamba alihadaiwa na kudanganywa mbali na ndoto zake kuzama.
Muda ulipozidi kusonga huku wakala asijulikane aliko, Davis hakuwa na chaguo jingine ila kujisakia malazi pekee yake, huku akisalia na matumaini kwamba huenda wakala huyo angemfikia.
Hata hivyo, kadiri siku zilivyogeuka kuwa majuma na majuma kuwa mwezi, ilibainika wazi kwamba ahadi hiyo kumbe ilikuwa bandia.
Hatimaye, baada ya kukata tamaa na kukatikiwa na raslimali, Davis alilazimika kuwasiliana na Chama cha ustawi wa wachezaji wa soka nchini Kenya (KEFWA), huku chama hicho kikichojitolea kumnasua kutoka utapeli huo.
"Nilivyoshindwa kuhimili yaliyonikuta, niliwaandikia Kefwa, walionisikiliza na kunisaidia. Walinihakikishia kwamba kila kitu kingekuwa sawa, maadamu ningeshirikiana nao vyema kuhusu hali yangu", Davis aliongeza.
Mchezaji huyo mwenye Umri wa miaka 22 alichezea klabu ya Nairobi City Stars katika kampeni ya ligi kuu ya 2020/21, tangu alipojiunga nao mnamo Januari 2017 kutoka Vapor Sports na alikuwa mfungaji bora wa klabu katika misimu tofauti. Pia amewahi kuichezea klabu ya Thika United
"Wachezaji wanapaswa kuangalia historia ya wakala, wateja wao wa zamani, na ushuhuda. Mawakala wa kweli wamesajiliwa na mashirika ya mpira wa miguu kama FIFA, UEFA, au vyama vya kitaifa vya mpira wa miguu. Wachezaji wanaweza kuthibitisha habari hii kwenye tovuti rasmi ili kuhakikisha wakala wanaowasilina nao wana mamlaka ya kuwawakilisha, " alibainisha rais wa Kefwa James Situma.
Kwa upande wake, katibu mkuu wa Kefwa Dan Makori amewatahadharisha wachezaji dhidi ya mawakala bandia wanaotoa ahadi au dhamana zisizo za kweli.
"Tunawahimiza wachezaji kukaa chonjo, kufanya utafiti wa kina, na kutafuta ushauri wa kisheria kabla ya kushirikiana na mawakala ili kuepuka kuangukiwa na kashfa, " alisema.
"Mawakala wa hakika huzungumza kwa uaminifu juu ya changamoto na uhakika katika tasnia ya mpira wa miguu, wakiepuka kuwapa wanasoka matumaini ya uwongo na madai ya kupindukia," alisisitiza, akiongeza kuwa kampeni dhidi ya mawakala bandia itaendelea.
Aidha, chama cha Kefwa, kwa kushirikiana na mashirika kama vile FIFPRO, wakfu wa Didier Drogba, na shirika la kimataifa la Kazi (ILO), kimekuwa kikifanya kazi kwa bidii kupambana na tishio la mawakala bandia kupitia hatua za udhibiti, kampeni za elimu, na mahitaji magumu ya leseni kwa mawakala wa wachezaji.