Harambee Stars yawanyamazisha wakosoaji wake kwa ushindi wa 5-0 dhidi ya Shelisheli. Picha: Shirikisho la soka. 

Timu ya Taifa ya Soka ya Harambee Stars imesajili ushindi wake wa kwanza kwenye michuano inayoendelea ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 kwa kuifunga Shelisheli 5-0.

Ushindi huo uliiwezesha Kenya kuchupa hadi nafasi ya tatu Kundi F, baada ya kukusanya pointi tatu na magoli muhimu kwenye mechi yake ya pili.

Mshambuliaji matata Michael Olunga, aliiweka Kenya kifua mbele kwa mabao mawili ya haraka, na kutuliza nyoyo za mashabiki wa Harambee Stars kabla ya Masud Juma kuzidisha uongozi wa Kenya hadi 3-0 kabla tu ya mapumziko.

Ushindi huo muhimu ulijiri kwenye mechi yake ya pili ya makundi, iliyopepetwa, Jumatatu, tarehe 20 Novemba 2023, uwanjani Stade Felix Houphouet-Boigny Mjini Abidjan, Ivory Coast.

Aidha, matokeo hayo yalimwezesha kocha wa Harambee Stars Engin Firat na kikosi chake kuwanyamazisha wakosoaji wake waliokuwa wakiitilia shaka safari nzima ya timu hiyo ya taifa.

Engin Firat

Kocha Firat alifanya mabadiliko kwenye safu ya kwanza ya mechi hiyo dhidi ya Shelisheli.

Kenneth Muguna na Abud Omar walioanza mechi dhidi ya Gabon, waliwapisha Eric Johanna na Eric 'Marcelo' Ouma.

Kenya ilizidi kuishambulia Shelisheli baada ya mapumziko, baada ya Rooney Onyango kufungua akaunti yake kwa bao lake la kwanza kwa timu ya taifa kupitia dakika ya 62.

Nyota wa klabu ya Gor Mahia, Benson Omalla alimridhisha kocha Firat kwa kumshirikisha kikosini baada ya kumaliza kibarua cha Harambee stars kwa bao la tano na la mwisho dakika ya 73.

Kenya sasa inasubiri kuialika Côte d'Ivoire mwaka ujao kwa mechi yake ya tatu ya michuano ya makundi ya kufuzu kwa Kombe la dunia 2026.

Kikosi cha Kenya kilichoanza mechi: Patrick Matasi (mlindalango), Eric Ouma, Amos Nondi, Johnstone Omurwa, Dennis Ng’ang’a, Anthony Akumu, Richard Odada, Rooney Onyango, Eric Johanna, Masud Juma, Michael Olunga

TRT Afrika