"Mliiona Simba iliyopambana na Wydad Casablanca robo fainali ya ligi ya mabingwa Afrika, CAF. Ingawa tumepoteza ngarambe hiyo 4-3 kupitia penalti, Simba imepokea heshima. Kwa sasa tayari nimeimarisha kikosi na huu ndio msimu wetu." Robertinho alisema.
Kocha wa Simba, Roberto Oliveira Goncalves do Carmo, 'Robertinho' anasema umiliki wa Yanga wa taji la ligi kuu ya bara ni wa mpito kwani wenyeji halisi wa Kikombe wamerejea. Baada ya kusalimu ligi kwa Yanga, na kufunga msimu uliopita kwa ukame, Robertinho amesema kuwa ni funzo tosha.
Robertinho, ambaye ataanza msimu wake kamili kama kocha wa wekundu wa msimbazi baada ya kujiunga nao mwezi Januari mwaka huu, ameeleza kuwa klabu hiyo imejiimarisha katika kila sekta kupitia uwindaji kamili waliofanya kwenye dirisha hili la uhamisho.
Samba huyo wa Simba, ameongeza kuwa likozi kwisha kwa wekundu wa msimbazi na ndio mwanzo wa kazi ya kuandika historia. Anadai kuwa huu si msimu wa visingizio tena kwani klabu hiyo imewekeza ipasavyo ikiwemo kuweka kambi ya hali ya juu nchini Uturuki.
Timu hiyo ilicheza mechi mbalimbali za kirafiki nchini Uturuki dhidi ya Turan PFK ya Ligi Kuu ya Azerbaijan, Adana na Eyupspor, Zira FC, na Batman Petrolspor A.S.
Mnyama alipoteza taji la ligi msimu uliopita kwa alama 5 pekee kwa kufungwa mechi moja na kutoa droo mechi 7.
Amefichua kuwa Rais wa Heshima wa klabu hiyo Mo Dewji amekuwa kiungo muhimu katika kuimarisha timu hiyo kwani uwekezaji alioufanya msimu huu, umeinua kiwango ya timu hiyo.
"Ninamshukuru sana Mo Dewji. Kwa hakika amenipa sikio na kufanikisha mapendekezo niliyotoa kwa klabu katika kila sekta ya timu." Robertinho alisema.
Miongoni mwa miamba hatari waliotinga kwa mnyama ni mchezaji bora msimu huu kwenye ligi kuu ya soka Rwanda Willy Essomba Onana pamoja, nyota wa Cameroon Che Malone Fondoh na straika wa zamani wa Asec Mimosas na raia wa Ivory Coast Aubin Kramo.
Mshambuliaji wa kimataifa wa Msumbiji Luís Miquissone pia amerejea kutoka Al Ahly kuchangamsha safu ya ufungaji ya Msimbazi.
Robertinho, alijiunga na timu hiyo katikati ya msimu na kuiongoza zikiwa zimesalia mechi 11 za ligi.
Uwekaji historia kupitia soka yenye mvuto sio jambo gumu kwa 'Robertinho', kwani aliisaidia Rayon Sports kutwaa mataji manne ya ligi na kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la CAF 2017/18.
Aidha, Robertinho amefichua kuwa mbali na wachezaji, usajili wa wataalam mbalimbali wakiwemo Mikael Igendia ambaye ni meneja mpya wa timu na mkuu wa sayansi, kocha wa viungo Corneille Hategekimana, kocha wa magolikipa Daniel Cadena Ledesma, na mtaalamu wa tiba ya viungo Wycliffe Omom utachangia pakubwa ufanisi wao msimu huu.
Zimesalia chini ya majuma mawili kabla ya msimu mpya wa 2023/24 wa ligi kuu ya NBC premier League kuanza tarehe Agosti 15 2023 kabla ya kumalizika Mei 2024.