Wachezaji wa timu ya taifa ya Morocco wakiongozwa na Sofyan Amrabat Na Hakim Ziyech ni miongoni mwa wale ambao wametuma ujumbe wa pole kufuatia tetemeko la ardhi lenye uharibifu nchini Morocco.
Shirikisho la kandanda ulaya UEFA nalo limetangaza rasmi kuwa mechi zote zijazo za timu ya taifa na mashindano ya klabu yatashuhudia kimya kuwakumbuka waathirika wa tetemeko la ardhi la nchini Morocco
Klabu ya Real Madrid ilikuwa mojawapo ya vilabu vya soka vya kwanza kutuma pole.
''Real Madrid C. F, Rais wake na bodi ya wakurugenzi wanaelezea pole zao na mshikamano na waathiriwa wa tetemeko la ardhi huko Morocco. Klabu yetu inaongeza rambirambi zake kwa familia za marehemu na watu wote wa Morocco. Vivyo hivyo, tunawatakia waliojeruhiwa kupona haraka na tunasambaza nguvu zetu zote na mapenzi.
Mahasimu wa Real Madrid, FC Barcelona, nao walitumia mtandano huo wa X kuandika; Kutoka FC Barcelona, tunaelezea mshikamano wetu kamili na nguvu kwa waathiriwa wa tetemeko la ardhi ambalo limeathiri Morocco. 🙏
Klabu ya PSG iliandika kwenye X; Familia nzima Ya Paris Saint-Germain iko pamoja na marafiki wetu Wa Morocco kufuatia tetemeko la ardhi la kutisha. Rambirambi zetu kwa wale ambao wamepoteza wapendwa wao. Mawazo yetu yako pamoja nanyi. ❤️ 💙
Aidha, Klabu ya kiungo wa timu ya taifa ya Morocco Sofiane Amrabat, Manchester United, nayo iliandika hivi kwenye mtandao wa X;❤️ 🇲🇦. Nyoyo zetu ziko pamoja na waathiriwa wa tetemeko la ardhi la usiku mmoja katika milima ya juu ya Atlas ya Morocco.
Klabu ya Uturuki ya Galatasaray ilimsajili winga wa Morocco Hakim Ziyech hivi karibuni, nayo ilitumia kurasa zake za mtandao kuandika; Mawazo na maombi yetu yako pamoja na wale walioathirika na tetemeko la ardhi #Morocco. 🙏 🇲🇦
Klabu ya Ujerumani ya FC Bayern nayo haikuchelea kuachia salamu zake za rambirambi kwa raia wa Morocco. Mawazo yetu ya FC Bayern yako pamoja na waathirika na familia zao za maafa ya tetemeko la ardhi nchini Morocco.
Klabu ya Uhispania ya Sevilla FC, inayotumikiwa na mfungaji wa Morocco En-Nesyri, iliandika; Sevilla FC inataka kuonyesha upendo na mshikamano wake na watu Wa Morocco na wale wote walioathirika baada ya matukio makubwa ya saa chache zilizopita.
Aidha, klabu ya Inter Milan iliyokuwa ya zamani ya Achraf Hakimi wa timu ya taifa ya Morocco, iliandika; Inter inataka kutuma salamu zake za huruma kwa waathirika wa tetemeko La Ardhi Nchini Morocco. Mawazo yetu yako na kila mtu katika wakati huu mgumu na wa kusikitisha. #FCIM
Klabu ya Ufaransa ya Olympique de Marseille nayo ilichapisha katika mtandao wa X; Katika msiba huu mbaya, Olympique de Marseille inatuma mawazo yake ya dhati na inataka kutoa msaada wake kamili kwa watu wa Moroko na wale wote walioathiriwa na janga lililotokea jana usiku. 🇲🇦 💙
Ligi kuu ya Saudia nayo imeungana na Ulimwengu mzima kutuma pole kwa Morocco kufuatia tetemeko hilo la ardhi.
Shirikisho la Soka la FA ya Morocco nayo imeahirisha mechi ya kufuzu Kombe la AFCON 2023, iliyoratibiwa kuchezwa dhidi ya Liberia baada ya tetemeko hilo la ardhi kuacha vifo vya zaidi ya watu 1000 na kuwajeruhi mamia.