Uganda imeahidi kutekeleza ahadi zake katika kufanikisha kuandaliwa kwa kombe la taifa bingwa Afrika Afcon 2027, Afrika Mashariki.
Katika taarifa kwa waandishi wa habari, mkewe rais wa Uganda Janet Museveni amesema kuwa Uganda itahakikisha kujengwa na kukamilishwa kwa viwanja vinavyotakiwa kwa upande wake, kufikia hadhi ya kimataifa kuweza kuandaa mechi za kombe hilo.
Bi Museveni, ambaye pia ndiye Waziri wa Elimu na Michezo, alisema haya, baada ya kupokea mkataba ulioandaliwa wa kutoa ombi la pamoja la mashirikisho ya soka ya Afrika Mashariki ya kuandaa kombe hilo mwaka wa 2027.
Ujumbe wa Uganda ulisafiri baada ya kukutana na rais kuelekea Misri, kuungana na wenzao kutoka Kenya na Tanzania ka lengo la kuwasilisha ombi lao.
Mei 23 ndio siku ya mwisho kwa mataifa yenye nia ya kuandaa kombe hilo, kuwasilisha maombi yao kwa CAF.
Katika mradi walioupa jina la ‘Pamoja,’ – Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Afrika Mashariki kuandaa kombe hilo kubwa zaidi barani katika historia ya kombe hilo.
Miongoni mwa masharti ya kuandaa kombe hili, ni kwa nchi husika kuwa na viwanja sita, ambazo mbili kati yao zina uwezo wa kushikilia mashabiki 40,000 kwa wakati, mbili zingine ziwe na uwezo wa kushikilia mashabiki 20,000 na zingine mbili 15,000 kila moja.
CAF inatarajiwa kutangaza muandaaji wa kombe hili mapema ili kutoa fursa kwa mataifa ambayo hayana miundo mbinu ya kutosha kuweka mambo sawa kabla ya kombe hilo kufika.
Mbali na viwanja, nchi hizo zinatakiwa kuwa na uwezo wa mahoteli kupokea timu na maelfu ya mashabiki watakao hudhuria shindano hilo.
Wengine wanaotafuta fursa ya kuandaa shindano hilo ni Algeria, Botswana na Misri.