Timu ya Taifa ya soka ya Harambee Stars imefunga safari kuelekea Uturuki kwa ajili ya kambi ya mazoezi kabla ya kukwatuana na miamba wa Urusi mjini Antalya.
Kikosi hicho kikiwa ni pamoja na kocha mkuu Engin Firat, kiliondoka uwanja wa kimataifa wa ndege wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi leo alfajiri baada ya kocha Engin Firat kukamilisha kikosi chake.
Wakati huo huo, baadhi ya wachezaji wanaosakata soka ya kulipwa ughaibuni wanatarajiwa kujiunga na kikosi hicho wakiongozwa na nahodha na mfungaji wa timu hiyo, Michael Olunga, pamoja na Masud Juma, Joseph Okumu, Brian Mandela, Johnstone Omurwa, Eric Ouma, Amos Nondi, Richard Odada, na Teddy Akumu.
Mechi hiyo ya kirafiki ya Harambee Stars, ambayo ni ya tatu ndani ya wiki kadhaa, baada ya kucheza na Qatar ugenini na kuwa wenyeji wa Sudan Kusini, inatarajiwa kupiga jeki maandalizi ya timu hiyo ya mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia 2026 zitakazoanza mwezi ujao, Novemba.
Kenya imewekwa kundi moja pamoja na Côte d'Ivoire, Gabon, Gambia, Burundi, na Ushelisheli.
Aidha, Kocha Engin Firat ametaja Kikosi cha Harambee Stars cha wachezaji 23 wakataoshiriki mechi yao ya kirafiki dhidi ya Urusi, mjini Antalya.
Walinda lango: Patrick Matasi, Brian Bwire, Bryne Odiambo
Mabeki: Joseph Stanley Okumu, Brian Mandela, Johnstone Omurwa, Collins Sichenje, Erick Ouma, Rooney Onyango, Daniel Sakari, Vincent Harper, Amos Nondi
Viungo: Richard And, Anthony Akumu, Kenneth Muguna, Alpha Onyango, Ayub Timbe, Ovella Ochieng
Washambuliaji: Masoud Juma, Alfred Scriven, Cliffton Miheso, Moses Shummah, Michael Olunga