Timu ya Afrika Kusini ya Kombe la Dunia la Wanawake imeitwa "mamluki" na "wasaliti" waliposusia mechi ya kirafiki dhidi ya Botswana kabla ya pambano la kimataifa mwezi huu.
Siku ya Jumapili, Banyana Banyana walisema uwanja wa mechi katika kitongoji cha Tsakane, kilomita 50 kusini mashariki mwa Johannesburg, ni cha kiwango duni kuchezea.
Wamelalamika kuwa, kucheza katika uwanja wa udongo na nyasi kunaweza kuwasababishia majeraha, na kuhujumu mchezo wao katika Kombe la Dunia huko Australia na New Zealand ifikapo Julai 20.
Banyana pia walitaka kucheza mchezo wao wa mwisho wa maandalizi kabla ya kusafiri kwenda Oceania katika ukumbi wa kifahari zaidi kama vile Soccer City mjini Johannesburg au uwanja wa Orlando huko Soweto.
Maafisa wa soka waliwaita wachezaji, akiwemo kijana wa miaka 13, kutoka ligi ya ndani na kuchelewesha kuanza kwa mechi hiyo kwa saa moja kabla ya Botswana kuwanyonyoa wapinzani wao wasio na uzoefu na kushinda 5-0.
Wapinzani ‘wenye nguvu’ zaidi
Matokeo dhidi ya wapinzani walioorodheshwa nafasi ya 96 chini ya Afrika Kusini yalikuwa aibu kubwa kwani washiriki wa kikosi cha Kombe la Dunia walisema kabla ya kususia kuwa wanataka wapinzani "wenye nguvu".
Afisa wa ngazi ya juu wa Chama cha Soka cha Afrika Kusini (SAFA), ambaye aliomba kutotajwa jina, aliambia gazeti la kila wiki la City Press kuwa wachezaji walikuwa na tabia kama "mamluki" na "wasaliti".
Kando na hali ya uwanja, Banyana haijafurahishwa na utaratibu uliopo wa malipo kabla ya Kombe la Dunia, ambapo wamepangiwa kumenyana na Uswidi , Argentina na Italia katika Kundi G.
Kwa mujibu wa wachezaji hao, watapokea dola 30,000 kila mmoja kutoka kwa FIFA kwa kufuzu kushiriki Kombe la Dunia, lakini hakuna chochote kutoka kwa shirikisho la nyumbani, SAFA.
Banyana ilijibu kwa kukataa kutia saini kandarasi za kabla ya mechi, ikisema wanataka nyongeza ya $21,000 kwa kila mchezaji kutoka chama cha kitaifa, kulingana na ripoti.
Madai ‘yasiyoeleweka’
Afisa mkuu wa fedha wa SAFA Gronie Hluyo alisema: "Wachezaji wanakosa busara katika matakwa yao.
"Kile ambacho FIFA imejitolea kuwapa ni zaidi ya tulivyojitolea kwa timu yoyote ya taifa hapo awali, ikiwa ni pamoja na Bafana Bafana (timu ya kitaifa ya wanaume)."
Hluyo alisema kila mchezaji alipokea randi 20,000 (wakati huo dola 1,500) kwa ajili ya kushiriki Kombe la Dunia 2019 nchini Ufaransa, ambapo Afrika Kusini ilishindwa na Hispania, China na Ujerumani.
"Wanachopata sasa ni zaidi ya hapo, lakini bado hawajafurahi," aliongeza afisa huyo.
Fuji zote hizi za kulalamikia hadhi ya ukumbi na marupurupu zilikuja wiki moja baada ya kuripotiwa kuwa kulikuwa na fujo mjini Pretoria ambapo kikosi cha Kombe la Dunia kilitajwa.
Baadhi ya waalikwa wa kisiasa hawakujitokeza kwa tukio lililoonyeshwa moja kwa moja kwenye kituo cha utangazaji cha serikali SABC, mfumo wa sauti haukufanya kazi vizuri, na skrini za jukwaa zilikosa kuonyesha chochote.
Banyana wanatarajiwa kusafiri New Zealand kwa makundi mawili, Jumatano na Alhamisi, na kucheza na Costa Rica katika pambano la mwisho la kirafiki kabla ya kumenyana na Uswidi mjini Wellington Julai 23.