Timu ya taifa ya soka ya Tanzania, ‘Taifa Stars’ imepanga kundi moja la C, ikiwa pamoja na timu za Nigeria, Tunisia na Uganda baada ya droo ya AFCON 2025 iliyofanyika jijini Rabat nchini Morocco siku ya Januari 27, 2025.
Kwa upande mwingine, wawakilishi wengine wa Afrika Mashariki kwenye michuano hiyo DRC, wako kwenye kundi D ambapo watachuana na Senegal, Benin na Botswana ili waweze kuvuka hatua ya makundi ya michuano ya AFCON 2025 ambayo itaanza kutimua vumbi Disemba 21, 2025 hadi Januari 18, 2026.
Wenyeji Morocco, wao wamepangwa kundi A, wakiwa pamoja na Mali, Zambia na Comoro wakati Misri wapo kundi B pamoja na Afrika Kusini, Angola na Zimbabwe.
Kundi E litahusisha Algeria, Burkina Faso, Equatorial Guinea na Sudan wakati lile la F, litakuwa na Ivory Coast, Cameroon, Gabon na Msumbiji.