Simon Msuva wa 'Taifa Stars' aliweka kimiani bao katika dakika 61 na kuikatia Tanzania tiketi ya kushiriki michuano hiyo mikubwa barani Afrika./Picha:  @Tanfootball

Bao pekee la dakika 61, lililotiwa kimiani na mshambuliaji anayeichezea Al-Talaba Sports Club ya nchini Iraq, Simon Msuva imeihakikishia 'Taifa Stars' tiketi ya kushiriki Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025), yatakayofanyika mwakani nchini Morocco.

Matokeo hayo, yanaifanya Tanzania kuungana na DRC na Uganda kama wawakilishi pekee kutoka ukanda wa Afrika Mashariki katika michuano hiyo mikubwa barani Afrika.

Kabla ya mchezo huo, ambao ulifanyika katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, msimamo wa kundi H ulikuwa unaongozwa na DRC iliyokuwa na alama 12, ikifuatiwa na Guinea yenye 9, 'Taifa Stars' ikishika nafasi ya tatu kwa alama 7, huku Ethiopia ikiburuza mkia na alama1.

Hii itakuwa ni mara ya nne kwa Tanzania kushiriki michuano hiyo, ikiwa imefanya hivyo mwaka 1980, 2019 na 2023.

TRT Afrika