Wachezaji wa Simba, msimu uliopita. Picha: Simba FC

Hatimaye Klabu ya Simba kutoka Tanzania maarufu 'Wekundu wa Msimbazi', wametua Uturuki kuanza kambi ya maandalizi ya msimu mpya mjini Ankara baada ya kuwasili kutoka Oman kwenye safari ndefu na ya kupitia anga za mataifa matatu.

Hapo awali, meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alifafanua kuwa timu hiyo itakuwa Uturuki kwa muda wa majuma matatu kufanya matayarisho kabambe ikiwemo kupiga mechi za kirafiki na timu mbalimbali za Uturuki.

Miamba hao, wakiongozwa na Kocha Mkuu Roberto Oliviera ‘Robertinho’, wameimarisha maandalizi yao kwa kukamilisha usajili wa wachezaji na wasimamizi wapya kwenye benchi lake la kiufundi.

Licha ya kuchujwa 4-3 na Wydad Atheltic Club ya Morocco, kupitia penalti kwenye hatua ya robo fainali ya ligi ya mabingwa Afrika CAF, Simba, imeonyesha nia yake ya kujiandaa vikamilifu msimu ujao kwa kuwanasa mastaa wapya mapema.

Taarifa zaidi zinasema kuwa timu hiyo itapiga mechi za kirafiki katika miji mbalibali ukiwemo mji mkuu wa Ankara.

TRT Afrika