Rais wa zamani wa FIFA Sepp Blatter amekosoa uamuzi wa shirikisho la soka duniani kuandaa kombe la dunia katika mataifa sita katika mabara matatu.
Morocco, Uhispania na Ureno zilitangazwa kuwa wenyeji wa michuano hiyo ya 2030, huku Uruguay, Argentina na Paraguay pia zikiwa mwenyeji wa mechi za ufunguzi kuadhimisha miaka 100 ya michuano hiyo, FIFA ilisema katika tangazo la kushangaza Jumatano.
Uamuzi huo ulikosolewa na Sepp Blatter, ambaye alikuwa Rais wa FIFA kuanzia 1998 hadi 2015, kabla ya kulazimika kutoka nje baada ya uchunguzi wa rushwa.
"Ni upuuzi kusambaratisha mashindano kwa njia hii," Blatter aliambia gazeti la Uswizi SonntagsBlick.
Sababu za kihistoria
"Fainali za Kombe la Dunia lazima ziwe tukio fupi la pamoja," alisema, akiongeza hii ilikuwa muhimu kwa utambulisho wa hafla hiyo, kwa shirika na kwa wageni.
Blatter, ambaye aliwahi kuwa mmoja wa vigogo wa soka, aliwahi kuikosoa FIFA kwa kuipa Qatar michuano ya 2022, akisema nchi hiyo ya Mashariki ya Kati ni ndogo sana.
kigogo huyo mwenye umri wa miaka 87 alisema mashindano ya 2030 yanapaswa kufanyika Amerika Kusini, kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 100 ya tukio la kwanza ambalo liliandaliwa na Uruguay ambao pia waliibuka mabingwa.
"Kwa sababu za kihistoria, Kombe la Dunia la 2030 lilipaswa kuwa la Amerika Kusini pekee," aliambia gazeti hilo.