Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akisalimiana na baadhi ya wachezaji wa timu ya Simba nchini humo mwezi Agosti mwaka jana. Picha/TRT Afrika. 

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amechangia shilingi milioni 500 za Kitanzania kutoka mfukoni mwake, ikiwa ni namna ya kuwezesha maandalizi ya ushiriki wa timu za taifa za nchi hiyo katika michuano ya Kimataifa.

Hatua hiyo inadhihirisha azma ya Serikali ya nchi hiyo katika kukuza maendeleo ya michezo na kuwawezesha wanamichezo kushiriki vyema katika mashindano mbalimbali ya kimataifa.

Mkurugenzi wa Hospitali ya Benjamen Mkapa, iliyopo Dodoma Dk. Alphonse Chandika. Picha/BMH

Rais Samia, ambaye alikuwa anazungumza kwa njia ya mtandao kwenye harambee maalumu ya kuchangia michezo nchini Tanzania, amesema mchango huo ni mwendelezo wa jitihada za Serikali katika kukuza michezo.

“Wakati vijana wetu wanapambana kutetea heshima ya nchi, ni vyema kukubali kwamba wanakutana na changamoto za rasilimali fedha,” alisema Rais Samia.

Katika kutambua mchango wa sekta ya michezo katika maendeleo ya taifa, Rais amewarai Watanzania kujitoa kwa hali na mali, kuchangia timu za Taifa zinazojiandaa na michuano ya Kimataifa.

Lengo la zoezi hilo, ambalo linaratibiwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ni kukusanya Shilingi bilioni 10, ambazo zitagawanywa kwa timu za Taifa zinazoshiriki michezo tofauti.

Zoezi hilo linakuja wiki moja kabla timu ya mpira wa miguu ya wanaume, maarufu kama Taifa Stars kutupa karata yake ya kwanza kwenye Michuano ya Kombe la Mataifa la Afrika (AFCON) 2023, yatakayoanza Jumamosi, nchini Ivory Coast.

Wakati huo huo, Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo jijini Dodoma nchini Tanzania imeungana na wadau wengine kuiunga mkono Timu ya Taifa ya Tanzania kwa kuchangia kiasi cha shilingi milioni 5.

Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Dk Alphonse Chandika amesema lengo la kuchangia ni kutoa hamasa katika michezo.

"BMH pia inapochangia timu za Taifa za Tanzania, imekuwa imehamasisha michezo kwa sababu michezo ni afay na unaposhiriki michezo unakuwa umeondoa uwezekano wa kupata magonjwa yasiyo yakuambukiza," amesema Dk. Chandika.

TRT Afrika