Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa timu hiyo kushiriki michezo ya olimpiki tangu kuorodheshwa kwa raga ya wachezaji saba kila upande . / Picha :  RUGBY Afrique     

Na Lynne Wachira

TRT Afrika, Nairobi, Kenya

Timu ya Afrika kusini ya wanawake katika raga ya wachezaji saba kila upande itashiriki michezo ya olimpiki mwaka ujao baada ya kufuzu kwa Michezo hiyo ya Paris kupitia ushindi wa 12-7 dhidi ya Kenya katika mashindano ya kombe la mataifa ya Afrika ambayo yamekamilika nchini Tunisia.

Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa timu hiyo kushiriki michezo ya olimpiki tangu kuorodheshwa kwa raga ya wachezaji saba kila upande katika michezo ya Olimpiki ya mwaka wa 2016 mjini Rio De Janeiro.

Afrika Kusini walikutana na Kenya katika fainlai na kuwavunjia matumaini ya kuweka historia kufuzu michezo ya Olimpiki kwa mara tatu mfululizo.

Bara Afrika itawakilishswa na Afrika kusini kwa upande wa wanawake na Kenya katika upande wa wanaume kwenye michezo ya Olimpiki mjini Paris/ Picha : Kenya Rugby Union

Timu zote mbili zilipimana nguvu vilivyo katika dakika sita za kwanza pasiwe na yeyote wa kuchukua uongozi. Afrika Kusina ilipata nafasi ya kupenya na kuchukua uongozi wa 5-0 sekunde chache tu kabla ya muda wa mapumziko kupitia Nadine Roos.

Katika kipindi cha pili, Kenya ilionekana kuwa na nguvu mpya huku Sharon Auma akiwapita kwa kishindo walinzi wawili wa Afrika kusini na kupachika try ya kwanza ambayo ilipata alama tatu zaidi kupitia Grace Okul, basi Kenya ikachukua uongozi wa 7-5 dhidi ya Afrika kusini.

Dakika zilizofuata zikawa ni za vuta ni kuvute lakini ikiwa imesalia takriban dakika moja kipenga cha mwisho kupulizwa, Afrika Kusini ikajikakamua na kufunga try kupitia kwa Maria Tshiremba na kufanya mambo kuwa 12 -7.

Kipenga cha mwisho kikapulizwa muda mfupi baadaye, na ikawa ni sherehe kwa Afrika kusini, ishara tosha kuwa kufuzu kwa Olimpiki ni mafanikio makubwa haswa baada ya timu ya wanaume kubanduliwa na Kenya ambayo ilifuzu kwa Olimpiki.

Hivyo basi bara Afrika itawakilishswa na Afrika kusini kwa upande wa wanawake na Kenya katika upande wa wanaume kwenye michezo ya Olimpiki mjini Paris mwaka ujao.

Fursa ya kufa-kupona kufuzu Olimpiki

Wakati uo huo, Kenya itapata nafasi ya mwisho ya kujaribu kufuzu kupitia mashindano ambayo huzileta pamoja timu zilizomaliza katika nafasi ya pili kwenye mashindano ya mabara.

Kenya Lioness, walishinda mecho zao zote kabla ya kuingia fainali / Picha : Kenya Rugby Union

Timu hiyo maarufu kama Kenya lionesses ilifuzu kwa nusu fainali baada ya kuzishinda mechi zake zote (Kenya 27 - Zambia 0, Kenya 41 - Ghana 0 na Kenya 20 - Madagascar 17).

Katika mechi ya nusu fainali dhidi ya majirani Uganda, lionesses waliweka wazi nia yao ya kufuzu kwa fainali kupitia kwa juhudi za mchwa kutoka kwa Janet Okello ambaye alifunga try tatu za kwanza na kuiweka Kenya mbele 17- 0 kufikia muda wa mapumziko.

Naomi Amuguni na Sharon Auma walifunga try kila mmoja na kuipa Kenya ushindi mkubwa wa 27- 0 dhidi ya Uganda.

TRT Afrika