Picha ya Rebecca Cheptegei ilionekana kwenye skrini kubwa baada ya mashindano ya Paralimpiki ya Walemavu siku ya Jumapili katika kumuenzi mwanariadha wa Uganda aliyefariki siku ya Alhamisi, siku nne baada ya kumwagiwa petroli na kuchomwa moto na mpenzi wake nchini Kenya.
Watazamaji walipiga makofi huku uso wa Cheptegei, ambaye alishiriki katika mbio za marathon za Olimpiki za Paris, ukionyeshwa kwenye Esplanade des Invalides.
Cheptegei alifariki katika shambulizi la hivi punde katika kinachoonekana kuwa msururu wa mashambulio dhidi ya mwanariadha wa kike nchini Kenya.
Cheptegei, 33, aliungua hadi zaidi ya 75% ya mwili wake katika shambulio la Jumapili, vyombo vya habari vya Kenya na Uganda viliripoti.
Ni mwanaspoti mashuhuri wa tatu kuuawa nchini Kenya tangu Oktoba 2021.
Siku ya Ijumaa, meya wa Paris alisema mji mkuu wa Ufaransa utamheshimu Cheptegei kwa kutaja kituo cha michezo kwa heshima yake.