Kipchoge  / Photo: AP

Na Yusuf Dayo

“Ni muhimu kushinda, lakini pia ni bora kushiriki na kumaliza mashindano”

Ndio usia kutoka kwa mwanariadha Eliud Kipchoge akiongea na wanahabari baada ya shindano la Boston Marathon.

Kwa mtu aliyezoea kushinda, kutokea nambari sita katika shindano hilo la Jumatatu 17 Aprili, lilikuwa pigo kubwa sio kwake tu bali pia kwa mashabiki wake duniani.

Muda wa 2:09:23 haikuwaridhisha wengi, ambao walibakia kujiuliza nini kilitokea?

“Nilipata matatizo mguuni baada ya kilomita 30, na nikajiambia siwezi kuacha.” Alisema Kipchoge. Aliongezea kuwa hali ya hewa haikuwa na athari yoyote kwake.

Lakini baadaye zikafuata mbio za London Marathon. Gwiji Mo Farah alitawala mbio hizo ila kuishia kupewa kichapo na wadogo wake kama vile Kevin Kiptum, ambaye ana miaka 23 tu ambae aliweza kumaliza kwa muda wa pili bora duniani katika historia ya Marathon.

 Mo Farah

Lakini pengine swali muhimu ni je, umefika wakati wa kustaafu kwa kina Kipchoge, Farah na wengineo?

Jibu hapa litategemea unamuuliza nani...

Wilfred Bungei, ambaye ni mshindi wa zamani wa dhahabu katika mashindano ya olimpiki anaiambia TRT Afrika, uamuzi huu unategemea mwanariadha mwenyewe.

“Kwa mwanariadha yeyote wa kimataifa, ni muhimu kustaafu ukiwa katika kilele cha ushindani wako. Wakati ambapo bado una ushawishi mkubwa. Usisubiri hadi umedhoofika ndipo unaondoka.” Ameongezea. “Hata hivyo wanariadha wengi wanakosa mpango na maandalizi muafaka ya kustaafu. Hawaelewi cha kufanya baada ya mchezo waupendao zaidi kumalizika.”

Naye bingwa wa zamani Douglas Wakiihuri anasema kuwa ni muhimu pia kwa mwanariadha kuusikiliza mwili wake.

Bolt 

“Inategemea ni mazoezi ya aina gani amekuwa akifanya au mashindano gani amekuwa akishiriki. Huenda mwili wako ukachoka kupita kiasi au ukapata jeraha na kulazimika kustaafu.”

Kuna baadhi ya wanariadha wanao ng’ang’ania mashindano kutokana na msukumo kutoka kwa mawakala au wadhamini. Wilfred Bungei ambaye alitangaza kustaafu punde baada ya kushinda mbio za Olimpiki mwaka 2009 anakumbuka alivyopokea kejeli awaeleza .

“Watu wengi walielezea kutoridhishwa, hasa wakala wangu. Bado alikuwa na matumaini ya kupata udhamini zaidi. Alitaka niendelee kwa muda zaidi.” Aliongezea, “Inategemea pia nini kinacho kusukuma. Una malengo gani. Tazama mfano Hicham El Guerrouj au Usain Bolt. Nina uhakika wakati wao wangelitaka kushindana mara moja nyingine wangemudu lakini walichukua uamuzi muafaka kwa wakati muafaka.”

Lakini Wakiihuri ambaye amewahi kushinda London Marathon, ubingwa wa dunia, New York Marathon na nyinginezo, alituambia TRT Afrika, wakati mwingine ni bora kuwaachia vizazi vipya nafasi. “ Ni lazima ukumbuke kuwa vijana wadogo zaidi wanakuja. Kwa hiyo ushindani unakuwa mkali zaidi. Licha ya kuwa bingwa wa dunia au mshindi wa dhahabu itakuja wakati utashindwa kutetea taji lako”

 Gebrselassie

Mo Farah ni miongoni mwa wanariadha maarufu waliojaribu bahati yao kwa muda mrefu zaidi. Akiwa na umri wa miaka 40, na baada ya kumaliza wa tisa katika mbio za London Marathon, hatimaye ametangaza kustaafu punde baada ya mashindano ya Great North ya mwezi Septemba mwaka huu.

Na kwingineko macho yote yamemuelekea mpinzani wake mkuu Eliud Kipchoge kujua na yeye lini atanawa mikono au pengine bado atakimbizana kutafuta mataji mengine?

TRT Afrika